Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof.
Palamagamba Kabudi ameliambia bunge leo Mei 08, 2025 kuwa Serikali inayoongozwa
na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itawapa timu ya Simba SC ndege kuelekea
Morocco kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Baada ya mafanikio makubwa ya Simba na sasa inaingia kwenye
mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho linaloandaliwa na CAF, Simba
inakwenda Morocco kupambana na RS Berkane na Serikali ya Tanzania inayoongozwa
na Rais Dr Samia imefanya maamuzi ya kutoa ndege itakayoipeleka Klabu ya Simba
Morocco kwa ajili ya mchezo huo,” amesema Prof. Kabudi.
Amesema kwamba Serikali imefanya uamuzi huo ikiwa ni sehemu
za jitihada za Serikali za kuipunguzia Simba umbali wa safari na uchovu, Simba
SC kwenda Morocco kwa ndege ya abiria kungewafanya wazunguuke na kutumia muda
mwingi njiani kutokana na kulazimika kupita nchi tofautitofauti kwa ajili ya
kuunganisha ndege.
Hii sio mara ya kwanza kwa Rais Samia kuzisaidia timu za Tanzania Kimataifa (Simba na Yanga) ili kuhakikisha zinafanya vizuri na kuitangaza nchi. Mwaka jana Yanga ilipofuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Rais Samia alitoa ndege iliyoipeleka timu hiyo Algeria na kuirudisha Dar es Salaam.

0 Maoni