Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewahimiza wadau wa elimu barani Afrika kuendeleza mkakati na
ushirikiano utakaowezesha mageuzi ya kidigitali
katika sekta ya elimu.
Dkt. Biteko ametoa rai hiyo leo Mei 8, 2025 jijini Dar es Salaam
wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la 18 la eLearning Afrika.
“ Tanzania inaendeleza dhamira yake ya mageuzi ya kidigitali
katika elimu na tungependa kushirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo, sekta
binafsi na wanazuoni ili kufanya e-
learning kuwezeshwa kwa ghrama nafuu kwa wote ,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Tanzania imedhamiria kuongoza katika mageuzi
ya kidigitali barani Afrika ambapo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050
inatambua kuwa mageuzi ya kidijitali ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi,
maendeleo ya kijamii na ushindani wa kimataifa. Ili kufanikisha hili, Tanzania
imeandaa mifumo kadhaa ikwemo Sera ya Taifa ya TEHAMA na Mkakati wa Uchumi wa
Kidijitali Tanzania 2024-2034.
Dkt. Biteko amesema kuwa Mkakati wa Taifa wa Elimu ya
Kidijitali na Programu ya Tanzania ya Kidijitali zinalenga kuimarisha
miundombinu na huduma za kidijitali, kuhakikisha teknolojia muhimu, vifaa,
muunganiko na rasilimali za e-learning vinafika maeneo mbalimbali nchini, aidha
nchi zingine pia zitumie rasilimali zao katika kusaidia mageuzi ya kidijitali
katika nchi zao.
Amewahimiza wadau wa kongamano hilo kuwa ili mageuzi ya
kidijitali ya Afrika yaweze kufanikiwa, lazima kuwezeshwa kwa nguvu kazi yenye
ujuzi kuanzia umri mdogo. Tanzania imefanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya
Elimu na Mafunzo mwaka 2023 na kuwa ni mfano muhimu, ikisisitiza uendelezaji wa
ujuzi kuanza elimu ya msingi.
“Sera hii pia inakuza matumizi ya teknolojia za kidijitali
ili kukabiliana na upungufu wa walimu, kupanua upatikanaji wa elimu, na
kuboresha ubora wa kujifunza. Mbinu hii inawaandaa wanafunzi kwa ajili ya
baadaye na kuwawezesha waelimishaji kwa kuwapa zana bora za kufundishia katika
nyakati za kidijitali,” amesema Dkt. Biteko.
Pamoja na hayo amesema kuwa Afrika lazima iendelee kuboresha
mazingira kwa kampuni za kibunifu ya ndani kwa kuunda sera saidizi zinazokuza
ubunifu na ujasiriamali ili kusaidia kukuza masoko ya ndani kwa teknolojia zinazoweza kuhamishwa na kuwezesha mataifa ya Afrika kuongeza ufanisi
wa rasilimali, kupunguza ucheleweshaji na kuharakisha mageuzi ya kidijitali.
Pia amebainisha kuwa ni muhimu kwa Bara la Afrika
kuwabakisha wataalamu wenye ujuzi ndani ya Afrika na kushirikisha diaspora ili
kuchangia ukuaji wa bara hilo. Kwa kuifanya Afrika kuwa kitovu cha maendeleo ya
kiteknolojia.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Prof. Adolf Mkenda amesema Tanzania imeendelea kuwekeza katika matumizi ya
teknolojia katika sekta ya elimu kwa kuhamasisha matumizi ya akili mnemba
katika shule.
Ameongeza kuwa kupitia Kongamano hilo lilianza Mei 7, 2025
litatoa fursa ya kuimarisha na kukuza uhusiano na ushirikiano katika nchi za
Afrika sambamba na kuboresha sera na mifumo yake ya elimu ili kuendana na
teknolojia, ubunifu na hususan matumizi ya akili mnemba.
Akieleza kuhusu eLearning Afrika, Mwanzilishi mwenza wa
FIRCAD- Ghana, Dkt. Aida Opoku- Mensah amesema kuwa akili mnemba ina manufaa
makubwa kwa maendeleo ya ikiwa ni pamoja na kutumika kutatua changamoto na
kufanya shughuli kama binadamu.
Amesema akili mnemba imekuwa na umuhimu mkubwa katika maisha
ya kila siku ya mwanadamu kwa kusaidia pia katika ufanyaji tafiti mbalimbali.
Amezungumzia utayari wa Afrika katika matumizi hayo na
kusema kuwa baadhi ya nchi za Afrika zimekuwa na mwitikio wa haraka wa matumizi
ya akili mnemba kuliko nyingine kutoka na uwekezaji wake.
Ametolea mfano Kenya (m-shule) na Nigeria tayari inatumia
mifumo ya akili mnemba kwenye mifumo yake ya elimu na Tanzania kupitia ubongo
kipindi kinachoelimisha na kuburudisha.
Amebainisha matumizi makubwa ya akili mnemba nchini China
yamesaidia kukuza uchumi wake, aidha Afrika inatakiwa kuwekeza katika akili
mnemba ili kusaidia katika sekta mbalimbali
za elimu na miundombinu.
Kongamano na maonesho ya kila mwaka la eLearning Afrika ,
ambalo lilianzishwa mwaka 2005, ni tukio kubwa linalotoa fursa ya kubadilishana
maarifa kwa elimu ya kidijitali, mafunzo na ujuzi katika Bara la Afrika.




0 Maoni