Rais Mwinyi:Ushirikiano wa kuimarisha hifadhi ni nyenzo muhimu kwa nchi za SADC

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa ushirikiano wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuimarisha hifadhi zinazovuka mipaka ni nyenzo muhimu ya kuzifanya kuwa endelevu na zenye manufaa kwa kila nchi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 23 Mei 2025 katika kikao cha Wakuu na Viongozi wa Serikali wa nchi za SADC kilichofanyika jijini Harare, Zimbabwe, kilicholenga kujadili uimarishaji wa hifadhi hizo katika ukanda wa SADC, ambapo amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkutano huo  ni sehemu ya maadhimisho ya mafanikio ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mpango wa uhifadhi wa hifadhi zinazovuka mipaka kikanda.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa umefika wakati kwa sera za nchi wanachama kuendana na sera kuu za SADC katika biashara ya kaboni, pamoja na kubadilishana uzoefu badala ya kila nchi kuwa na sera tofauti kwa maslahi ya kikanda.

Aidha, amesema kuwa mkutano huo umeonesha dira na utayari wa SADC katika uhifadhi wa pamoja wa bahari, wanyamapori, rasilimali za maji, misitu, na kusisitiza zaidi katika uchumi wa buluu  eneo ambalo Zanzibar inalitegemea kwa kiasi kikubwa.

Vilevile, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuzishirikisha zaidi jamii, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, wadau na asasi zisizo za kiserikali katika kufanikisha azma ya pamoja ya uhifadhi.

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa nchi wanachama wa SADC kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina yao, kwani uhifadhi wa hifadhi zinazovuka mipaka unahitaji mshikamano wa kweli na juhudi za pamoja.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya SADC ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Dambudzo Mnangagwa, amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha wananchi ili nao wawe sehemu ya juhudi za pamoja za kuimarisha hifadhi zinazovuka mipaka na kuzifanya kuwa endelevu.



Chapisha Maoni

0 Maoni