Abidjan. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, ameongoza
mazungumzo ya kitaalamu kati ya Serikali ya Tanzania na Bw. Soren Toft, Afisa
Mtendaji Mkuu wa Mediterranean Shipping Company (MSC), kuhusu uwekezaji wa
kimkakati katika Bandari ya Dar es Salaam na Mangapwani–Zanzibar.
Mazungumzo hayo na kampuni ambayo makao yake makuu yapo
Geneva, Uswisi, yamefanyika jana jijini Abidjan, Côte d’Ivoire pembezoni mwa
Jukwaa la Maafisa Watendaji Wakuu Afrika, yakilenga fursa za kuboresha huduma
na miundombinu ya bandari hizo mbili muhimu kwa uchumi wa taifa na ukanda wa
Afrika Mashariki.
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kupitia kwa Mkurugenzi
wa Fedha na Utawala, Bw. Pascal Maganga, kimeihakikishia MSC kuwa kipo tayari
kushirikiana kikamilifu kwa kuhakikisha mazingira rafiki ya uwekezaji ili
uwekezaji huo ufanyike kwa mafanikio makubwa.
Kwa upande wake, Bw.Toft ameonyesha dhamira ya dhati ya MSC
kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha miundombinu ya bandari, akisisitiza
umuhimu wa Bandari ya Dar es Salaam na Mangapwani kama lango kuu la biashara
kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Tanzania inaendelea kujidhihirisha kama kitovu cha uwekezaji barani Afrika, kwa kushirikiana na wadau wakubwa wa kimataifa katika kuendeleza miradi ya kimkakati itakayochochea uchumi wa nchi na ajira kwa wananchi.




0 Maoni