Mwenyekiti wa kamati
ya Mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo na Mbunge wa Dodoma Mjini Mhe. Anthony
Mavunde jana amekabidhi matofali 41,000 na Saruji tani 102 kwa kata zote 41 za
Dodoma Mjini kwa lengo la kuunga mkono miradi inayoibuliwa na wananchi katika
ujenzi wa miundombinu ya Elimu na vituo vya Afya.
“Mfuko wa Jimbo
hujielekeza katika miradi ya kipaumbele ya Elimu, Afya na uwezeshwaji wananchi
kiuchumi.”
Leo tunakabidhi matofali
na saruji kwa kata zote 41 kwa lengo la kuunga mkono miradi inayoibuliwa na
wananchi.
Kwasasa Jiji la
Dodoma limetenga Shilingi Bilioni 6 kuunga mkono miradi yote inayoibuliwa na
wananchi ili kuchochea maendeleo zaidi ndani ya Dodoma Jiji.
“Mh. Rais Dkt. Samia
S. Hassan amefanya kazi kubwa sana ya kuiendeleza Dodoma hivyo ni wajibu kazi
hii nzuri kuungwa mkono kwa wivu mkubwa,” alisema Mavunde.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mh. Jabir Shekimweri na Mwenyekiti wa
CCM wilaya ya Dodoma Ndg. Charles Mamba wamepongeza hatua ya Mfuko wa Jimbo
kujibu mahitaji ya jamii na hasa katika kuboresha sekta ya Elimu na Afya na
hivyo kusaidia kusogeza maendeleo kwa wananchi kwa ukaribu zaidi.
Akitoa taarifa ya
mfuko wa Jimbo,Mratibu wa Mfuko Bi. Debora Muwinje amesema mfuko wa Jimbo la
Dodoma Mjini unapokea kiasi cha Shilingi Milioni 93 kuchochea maendeleo kiasi
ambacho kimetumika na kugharamia mahitaji ya vifaa husika na kumpongeza Mbunge
Mavunde kwa kuchangia mifuko ya saruji 1000 ya ziada ili kuhakikisha eneo kubwa
zaidi linaguswa.
0 Maoni