MAKUSANYO ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa wa Ruvuma yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali kwa mwaka wa fedha ulioanza Julai 2024/2025 ni Shilingi Bilioni 32.5.
Fedha hizo ni makusanyo ya mpaka tarehe 19 Mei, 2025 wakitarajiwa
kuvuka lengo la fedha walilopangiwa la Shilingi Bilioni 33.15.
Akizungumza na
wanahabari wa Tume ya Madini, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma,
Mhandisi Alphonce Bikulamchi amesema, hadi mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu
Mkoa huo utakuwa umevuka lengo la zaidi ya
asilimia 100 ya ukusanyaji
mapato.
Mhandisi Bikulamchi amesema kuwa mafanikio hayo yamepatikana
kutokana na kushamiri kwa biashara ya makaa ya mawe ambayo kwa Mkoa wa Ruvuma
yamebainika kuwa ni bora zaidi na yamekuwa yakiuzwa nchi mbalimbali ikiwemo
Kenya, Uganda, Rwanda, Bara la Asia na Bara la Ulaya.
Aidha, amesema pia Mkoa huo mbali na makaa ya mawe pia umebarikiwa kuwa na aina nyingi
za madini ikiwemo Dhahabu, Shaba, Chuma,
Urani, Madini ya Ujenzi na Madini ya Vito.
Amesema pia kuna masoko mawili ya madini ambayo ni Soko la
Madini Songea na Soko la Madini Tunduru ambayo yalianzishwa na Serikali kupitia
Tume ya Madini ili kuongeza uwazi, usawa, ulinzi wa haki halali na maslahi ya
watu wanaofanya biashara hiyo huku akiwataka watanzania kuchangamkia fursa
mbalimbali zilizopo mkoani humo kama usambazaji wa teknolojia zinazotumika
migodini, usambazaji wa bidhaa za vyakula, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya
madini.






0 Maoni