WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo iimarishe na kufanya ufuatiliaji wa Watendaji wa Vyama vya Ushirika ili wazingatie maadili ya utumishi wa ushirika, uwazi, uwajibikaji na utawala bora, na hivyo kuwavutia wanachama na wawekezaji.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo, pamoja
na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, iharakishe na kusimamia kikamilifu
utekelezaji wa mikakati yote iliyopitishwa, hususan katika maeneo ya teknolojia
ya kilimo, upatikanaji wa pembejeo, na masoko ya mazao.
Ametoa maagizo hayo jana alipozindua mdahalo wa Upatikanaji
Mitaji ya Fedha za Maendeleo ya Ushirika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya
Kikwete, jijini Dodoma. Pia, Waziri Mkuu amezindua ripoti ya Mwaka ya Kilimo kwa
mwaka 2022/2023, 2023/2024.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuzisisitiza taasisi za
kifedha, zikiwemo benki na mifuko ya maendeleo, ziendelee kushirikiana kwa
karibu na vyama vya ushirika kwa kuweka mifumo rafiki ya upatikanaji wa mikopo
na mitaji kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo.
Mheshimiwa Majaliwa amewataka wakulima na wananchi kwa
ujumla wahakikishe wanajiunga na vyama vya ushirika vilivyosajiliwa, ili waweze
kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo.
“Wadau wote wa maendeleo, endeleeni kushirikiana na Serikali
katika kutoa rasilimali, utaalamu na ubunifu unaohitajika katika kuendeleza
sekta hii muhimu. Wizara ihakikishe maandiko ya taarifa zilizozinduliwa
zinaandaliwa pia kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi
kunufaika nazo.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Sekta ya Ushirika nchini
inaendelea kuimarika kwa kasi, ikiwa ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi
na kijamii, hasa katika maeneo mbalimbali.
“Hadi sasa, Tanzania inajivunia kuwa na zaidi ya vyama 7,000
vya Ushirika vilivyosajiliwa, vyenye jumla ya wanachama zaidi ya milioni nane.
Vyama hivi vinajumuisha sekta mbalimbali za uchumi kama vile kilimo, uvuvi,
madini, biashara na huduma za kifedha.”
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua madhubuti za kuleta mageuzi
katika Sekta ya Ushirika ikiwemo kuboresha mifumo ya usimamizi na uendeshaji wa
vyama vya ushirika pamoja na kuimarisha masoko ya mazao kupitia mfumo wa
Stakabadhi za Ghala.
“Kuwapatia Maafisa Ushirika vitendea kazi ili waweze
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kuboreshwa kwa upatikanaji wa pembejeo kwa
wakulima kupitia vyama vya ushirika na kuimarishwa kwa huduma za kifedha
kupitia kuanzishwa kwa Benki ya Ushirika (COOP Bank).”
Akizungumzia uzinduzi
rasmi wa mradi wa Mashamba Makubwa unaofadhiliwa kwa pamoja na Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania, Waziri Mkuu amesema mradi
huo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya BBT.
“…mradi ambao nimeuzindua leo, utatekelezwa kwa kipindi cha
miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030. Gharama ya jumla ya utekelezaji wa
BBT Project 1 ni Dola za Marekani milioni 241.27, ambapo AFDB itachangia Dola
milioni 129.71, sawa na asilimia 53.76 ya gharama hiyo. Serikali ya Tanzania
itachangia asilimia 46.24 ya mahitaji hayo ili kukamilisha mradi huu.”
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema
ushirika ni njia pekee inayowajengea uimara wanaushirika na kwamba benki ya
ushirika inakwenda kurahisisha malipo ya wakulima. Benki ya Ushirika inamtaji
wa zaidi ya shilingi bilioni 50 na itakuwa na mawakala zaidi ya 50 nchini.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Ushirika
(Coop Bank), Profesa Gervas Machimu amesema benki hiyo itakuwa nguzo ya
maendeleo ya ushirika mijini na vijijini, itarudisha heshima ya ushirika na
kuchochea uchumi wa wananchi.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni ya Tume ya Vyama vya Ushirika, Abdulmajid Nsekela alisema Benki ya Ushirika itaendeshwa kisasa zaidi na itakuwa na ushindani na kutoa taswira ya ushirika wenye tija.



0 Maoni