Wanawake nchini Tanzania wametajwa kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 35 ya uchumi wa Tanzania unatokana na juhudi za wanawake ambao wanachangia asilimia 70 ya nguvu kazi ya kilimo ni wanawake hasa katika mazao ya chakula.
Mchango wa mwingine wa
wanawake unajidhihirisha katika biashara, viwandani na katika huduma za kifedha
kupitia utafiti uliofanywa na Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) mwa ka 2022 umeonesha
wanawake ni 47% ya wafanyakazi wote wa sekta ya fedha. Pia wanashika 10% ya
nafasi za kufanya maamuzi. Vile vile, 18% wakiwa wajumbe katika bodi za
wakurugenzi sawa na wastani wa wanawake wawili katika kila bodi.
Hayo yamebainishwa leo
Aprili 14, 2025 jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.
Dkt. Doto Biteko wakati aliposhiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa
Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA).
Pamoja na mafaniko hayo,
Dkt. Biteko ametaja changamoto zinawakabili wanawake katika sekta ya fedha kuwa
ni uhaba wa upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu, elimu duni ya masuala ya
kifedha na uchache wa nafasi za kushiriki katika maamuzi ya Sera za Fedha.
Amewanawake nchini
kuzingatia misingi ya malezi kwa watoto wao kwa kuwapa nafasi sawa watoto wa
kike na wa kiume ili kukabili changamoto zinazotokana na mila, desturi
utamaduni.
“ Kwa kushirikiana na wadau
wengine Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua
hatua za makusudi ili kutatua changamoto zinazomkabili mwanamke na hivyo
kuchochea maendeleo" amesema Dkt. Biteko.
Amebainisha baadhi ya hatua
hizo kuwa ni kuwaamini na kuwapa
wanawake nafasi za juu za uongozi na maamuzi, kufanya Mapitio na Tathmini ya
Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2000, kuandaa miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Ulinzi na Usalama wa Wanawake na
Vijana Vyuoni uliozinduliwa mwaka 2023 na kutoa fursa nyingine mbalimbali za
kifedha na kiuchumi kwa wanawake.
Amesisitiza kuwa wanawake
wanatakiwa kuwekeza zaidi katika mifumo ya kidigitali ili kuendana na mabadiliko
ya kidigitali "Naomba hapa nitoe rai kwenu kuwa, mkiwa mnaendelea
kutekeleza majukumu yenu, msisahau kuhusu kuwekeza katika teknolojia. Maana
Dunia ya sasa inazidi kwenda zaidi katika maisha ya kidigitali. Hii itasaidia
kurahisisha biashara na kufikisha huduma kwa wepesi hususan katika maeneo ya
vijijini,”
Fauka ya hayo, Dkt. Biteko
amesema kupitia mijadala na maazimio yatakayotolewa katika mkutano huo,
zitapatikana mbinu mpya za kuongeza
ushiriki wa wanawake katika sekta ya fedha na uchumi wa nchi kwa ujumla kupitia
mabenki, kampuni za bima, masoko ya mitaji. Pamoja na mbinu na njia mbalimbali
za fedha mtandao zinazotatua changamoto zinazomkabili mwanamke katika sekta ya
fedha.
Naibu Waziri wa Wizara ya
Fedha, Mhe. Hamad Chande amewapongeza wanawake nchini kwa kuanzisha Chama hicho
kinacholenga kusaidia wanawake kiuchumi.
Amewahakikishia kuwa
Serikali imeandaa mazingira rafiki kwa wanawake katika ukuzaji wa uchumi “
Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa kutunga sera na sheria za kiuchumi ili
wanawake na makundi mbalimbali yaweze kuimarika kupitia taasisi na vyama kama
hivi. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana nanyi ili kuimarisha TAWiFA ili
kuhakikisha nafasi ya mwanamke inazidi kuwa juu katika jamii.”
Rais wa Chama cha Wanawake
katika Sekta ya Fedha (TAWiFA), Fikira Ntomola amesema kuwa wanawake nchini
wameendelea kujishughulisha ili kuhakikisha sekta ya fedha nchini inakuwa.
Aidha, jamii inapaswa itambue uwekezaji kwa wanawake si hisani bali ni
uwekezaji wa kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.
“ Tunaahidi kufikisha elimu
ya fedha kwa wanawake katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuandaa mafunzo na
warsha kwa lengo la kuongeza uwezo wa kusimamia masuala yao ya fedha na
biashara,” amesema Bi. Ntomola.
Ameongeza kuwa TAWiFA
imedhamiria kuleta mabadiliko chanya kuhusu ushiriki wa wanawake katika sekta
ya fedha, aidha wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka sera na sheria
zinazochochea uchumi jumuishi na uwepo
wa usawa wa kijinsia kiuchumi na kijamii.
“Tumekuwa tukiwajengea uwezo
wanawake wa kuendesha biashara zao kiufanisi, kukuza biashara zao na
kupanua wigo wao kuhusu sekta ya fedha,”
amebainisha Bi. Ntomola.
Amewaomba wadau mbalimbali
nchini kufungua milango ya fursa kwa wanawake, na kuwa TAWiFA ipo tayari
kushirikiana nao kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa umma, pamoja na tafiti
za kuendeleza miradi ya kusaidia wanawake ili kujenga sekta ya fedha iliyo
jumuishi.
Makamu wa Rais wa Chama cha
Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWIFA), Nangi Massawe amesema kuwa Chama hicho
kinakutanisha wanawake katika sekta ya fedha ili kujenga sekta yenye usawa kwa
manufaa ya Taifa.
TAWiFA kina jumla ya
wanachama 204 na kimeendelea kuhakikisha wanawake wanashiriki katika sekta hiyo
ili kuchochea maendeleo.
0 Maoni