Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Mhe. Hamza S. Johari amewaongoza Mawakili wa Serikali kushiriki katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali unaofanyika Jijini, Dodoma tarehe 14 hadi 15 Aprili, 2025.
Akizungumza katika Mkutano
huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewataka Mawakili wa Serikali kuutumia
mkutano katika kujadili kwa kina masuala mbalimbali yanayohusu Chama cha
Mawakili wa Serikali pamoja na Sekta ya Sheria kwa ujumla.
“Wote tunafahamu lengo la
mkutano huu ni kutoa fursa kwa wanachama kujadili mambo mbalimbali yanayohusu
chama chetu.”
Katika hatua nyingine, Mhe.
Johari amewakumbusha Mawakili wa Serikali kuendelea kutekeleza majukumu yao
vizuri ili kuweza kuifikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, kwa kuzingatia na kuiishi kauli mbiu ya
mkutano huo inayosema “Utawala wa Sheria katika utekelezaji wa majukumu ya
Serikali, ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo
2050.”
“Kauli mbiu yetu ya Mwaka
huu imejielekeza kwenye Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 na ili tuifikie dira hii
tunatakiwa kuwa na proper legal framework na sisi tunataka kuwa facilitator wa
kulifikisha taifa huko.”
Awali, akimkaribisha
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel
M. Maneno amewahakikishia Mawakili wa Serikali kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Mawakili wa Serikali wanaendelea kutekeleza
majukumu yao kwa ujasiri na ulinzi mkubwa bila kutetereka.
“Tutahakikisha kila Mwanasheria
kule aliko anatekeleza majukumu yake kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
na milango ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu iko wazi wakati wowote tutawasikiliza.”
Kwa upande wake, Naibu
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Ndg. Shaaban Ramadhan Abdalla ameishukuru Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania kwa
kuialika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kuja kuhudhuria Mkutano huo huku
akikipongeza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kuendelea kuwasimamia vizuri
Mawakili wa Serikali.
Mkutano Mkuu wa Chama cha
Mawakili wa Serikali umeanza tarehe 14 Aprili, 2025 kwa Mawakili wa Serikali
kupokea taarifa mbalimbali zinazohusu chama hicho na Mkutano utaendelea hadi
tarehe 15 Aprili, 2025 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Doto
Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Aidha, kupitia mkutano huo
Mawakili hao watapata fursa ya kufanya uchaguzi kwa kuwachagua viongozi
mbalimbali wa kukiongoza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kipindi cha mwaka
mmoja.
0 Maoni