WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amesema kuwa Tanzania itaendelea kushiriki na kutimiza matakwa ya kimataifa
katika kupambana na kudhibiti uhalifu wa kifedha.
Amesema kuwa Tanzania
inatambua changamato za uhalifu wa kifedha na imejidhatiti katika kudhibiti
hali hiyo kwa viwango vya kimataifa vilivyopo.
Amesema hayo leo Jumatatu
(Aprili 14, 2025) wakati Ufunguzi wa Mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na
Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kudhibiti Fedha Haramu, kwenye ukumbi wa Benki
Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa kufuatia
tathmini zilizofanywa na taasisi za Kuthibiti Uhalifu wa Kifedha Kusini
Mashariki mwa Afrika mwaka 2021 na Kikosi cha Kimataifa cha Ushirikiano na
Tathmini ya mwaka 2022, Tanzania imeimarisha mifumo ya kupambana na fedha
haramu ikiwemo kujengea uwezo wa rasilimali watu na vifaa taasisi zinazohusika
katika mapambano hayo.
Waziri Mkuu ameyataja maeneo
yaliyofanyiwa kazi kuwa ni mabadiliko ya sheria na sera, matumizi ya takwimu na
teknolojia, kuimarisha sekta nyumba na ardhi, kuwajengea uwezo wadau na
kuimarisha usimamizi wa Taasisi za za kifedha.
Kwa upande wake, Waziri wa
Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Tanzania baada ya kupokea mpango kazi
kutoka Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kupambana na Fedha Haramu ilifanya maamuzi
ya ngazi ya juu ya kuimarisha usimamizi uhalifu wa kifedha nchini hali ambayo
imeonesha mafanikio makubwa.



0 Maoni