Katika kuchukua hatua za
kudhibiti mwendo wa kasi kwa magari ya usafirishaji nchini Mamlaka ya Udhibiti
Usafiri wa Ardhini (LATRA), imeyaunganisha magari 11,826 kwenye mfumo wa ufuatiliaji
mwenendo wa safari (VTS) hadi kufikia Machi 2025.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar
es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini, CPA
Habibu J. Suluo katika mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari na LATRA, chini
ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Kati ya hayo, magari 8,969 yanayotuma taarifa
kwenye mfumo mpaka sasa. Pia, wastani wa magari 5,800 yanafanya safari kila
siku katika nchi yetu na idadi hiyo huongezeka katika kipindi cha mwisho wa
mwaka na hufikia mpaka magari 6,200 yanayofanya safari kwa siku,” amesema CPA Suluo.
Ameeleza kuwa katika magari
yasiyotuma taarifa, baadhi hayapo barabarani kutokana na sababu mbalimbali
kama, matengenezo ya muda mrefu, ajali, kuungua moto na baadhi yamebadili njia
(route) na kuhamia kwenye njia ambazo hazina uhitaji wa kufunga vidhibiti
mwendo (VTS).
Mfumo wa VTS unalenga
kusimamia matakwa ya usalama wa huduma kama ilivyoelekezwa kwenye Kifungu cha
5(1)(d) na Kifungu cha 6(g) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini,
Sura ya 413, LATRA.
0 Maoni