Miradi ya ujenzi wa madarasa mawili yenye thamani ya shillingi millioni 60 katika kijiji cha Ngumbu wilaya ya Liwale mkoani Lindi inayotekelezwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA chini ya ufadhili wa ushirika wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) na Tanzania umeibua matumaini mapya katika Sekta ya elimu Kwa jamii hiyo inayozunguka Hifadhi ya Selous.
Wakizungumza katika nyakati
tofauti Aprili 14, 2025 wananchi hao wamesema ujenzi wa madarasa utapunguza
uhaba wa miundombinu ya kielimu, kuongeza Ari ya kusoma na kuibua ndoto na matumaini mapya ya mafanikio ya kitaaluma kwa
wanafunzi.
"Sasa tunakwenda dunia
ya tatu, dunia inayomtaka mwanafunzi akae asome katika sehemu nzuri, apate
taaluma nzuri ili aweze kujifunza vizuri. Kwahiyo kitendo cha kupata haya
madarasa ninawashukuru sana TAWA na wafadhili wanaoshirikiana nao,"
amesema Mhe. Faraji Saidi Diwani wa Kata ya Kibutuka.
Kamanda wa TAWA Kituo cha
Liwale, Philipo Urio amesema mradi huo
umetokana na fedha za dharura za UVIKO 19 Kwa lengo la kusaidia shughuli
za uhifadhi katika Pori la Akiba Selous na Hifadhi ya Taifa Nyerere na kwasasa
umefikia asilimia 97 na unatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi huu wa Aprili
tayari Kwa kuanza kutumika rasmi.
Amesema Kijiji cha Ngumbu
kilichopo Kata ya Kibutuka kimezungukwa na Pori la Akiba Selous na hivyo kuwa
wanufaika wa moja Kwa moja na fursa zitokanazo na uhifadhi zinazolenga kujenga
uhusiano mzuri baina ya jamii na rasilimali za Taifa wakiwamo wanyamapori
hususani tembo.
Mkuu wa wilaya ya Liwale
Mhe. Goodluck Mlinga amepongeza jitihada za TAWA katika kuboresha huduma za
kijamii Kwa wananchi hatua ambayo inasaidia kuongeza uhusiano mzuri baina ya
wananchi na rasilimali za Taifa hususani wanyamapori.
"Hii itaisaidia nini?,
Kwanza wananchi kuheshimu wanyamapori maana mwanzoni wananchi walikuwa
hawahwshimu wanyama, wakiwaona wanajua ni maadui, lakini sasa hivi na wenyewe
wanashiriki kwenye uhifadhi. Lakini Pili wananchi watashiriki katika utoaji wa
taarifa za ujangili maana yake sasa wanaona wanyama ni Kinga Kwa ajili yao,"
amesema Mlinga.
Naye Katibu wa Mbunge wa
Liwale, Jaizu Abdallah ametambua mchango wa TAWA kwenye wilaya ya Liwale na
kusema kuwa kitendo cha kujenga vyumba
hivyo vya madarasa shule ya msingi Ngumbu ni hatua nzuri ya kuboresha mazingira
ya watoto kupata elimu bora.
Kwa upande wake Afisa Habari
wa TAWA Beatus Maganja ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na
Utalii Kwa kutoa mazingira wezeshi Kwa wadau mbalimbali wa uhifadhi Kwa jili
kutekeleza majukukumu yao hasa ya kiuhifadhi kama ilivyo Kwa Kijiji cha Ngumbu.
"Tuna kila sababu ya
kushukuru wadau wetu lakini pia Serikali Kwa namna inavyoshirikiana na wadau
hawa na leo tunaweza kuona matokeo makubwa ambayo yanatokana na hizi shughuli
ambazo zinafanywa na wadau wetu katika maeneo yetu. Kijiji cha Ngumbu sasa
kinashuhudia matokeo chanya ya jitihada za uhifadhi," alisema Maganja.
Mkuu wa wilaya ya Liwale Mhe. Goodluck Mlinga akiipongeza jitihada za TAWA katika kuboresha huduma za kijamii.
Kamanda wa TAWA Kituo cha
Liwale, Philipo Urio, akielezea mradi huo wa ujenzi wa madarasa mawili.
Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja akiwaelezea wananchi wa Liwale kuhusu manufaa yatokanayo na uhifadhi.
Madarasa mawili yenye thamani ya shillingi millioni 60 yaliyojengewa na TAWA katika kijiji cha Ngumbu wilaya ya Liwale mkoani Lindi.
0 Maoni