Wizara ya Maliasili na Utalii katika kipindi cha mwaka 2024/2025 imebaini vivutio vipya vya utalii 337 katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi na Kigoma.
Haya yamebainishwa Bungeni Dodoma
na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa
akijibu swali na Mhe. Prof. Patrick Alois Ndakidemi aliyetaka Kujua Serikali
ina mkakati gani wa kupanua wigo wa maeneo mapya ya utalii nchini.
Mhe. Kitandula aliongeza
kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na utalii imekuwa ikitekeleza
mikakati mbalimbali inayolenga kupanua wigo wa mazao ya utalii nchini ili
kuvutia watalii wengi zaidi, kuongeza siku za watalii kukaa nchini, kuongeza
mapato yatokanayo na shughuli za utalii pamoja na kupunguza utegemezi katika
zao la utalii wa wanyamapori nchini.
Vilevile Mhe. Kitandula
alisema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka sekta
za umma na binafsi kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo utalii wa
fukwe, meli, mikutano na matukio, malikale, utamaduni na michezo.
“Katika kuendeleza utalii wa
meli nchini, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau wa sekta binafsi wenye
mtandao mkubwa katika soko la kimataifa la utalii wa meli kutangaza zao hili.
Katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Machi, 2025, jumla ya meli za kitalii 9
ziliwasili nchini na kuleta watalii 2,944 waliotembelea vivutio mbalimbali vya
utalii,” alisema Mhe. Kitandula.
Na. Anangisye Mwateba -
Bungeni Dodoma
0 Maoni