Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa jana Aprili 8, 2025 ulishiriki Jukwaa Maalum la Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi zinazozalisha Madini ya Almasi Barani Afrika (The African Diamond Producers Association - ADPA Council Of Ministers).
Mkutano huo
unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Bintumani Mjini Freetown
nchini Sierra Leone unatarajia kuhitimishwa Aprili 11, 2025 huku agenda
mbalimbali zikitarajiwa kujadiliwa ikiwemo ya kupokea na kujadili taarifa ya
mapato na matumizi ya fedha ya umoja huo pamoja na sera mpya ya uchangiaji wa
ada kwa nchi wanachama.
Nchi
zinazounda jumuiya hiyo zinahusisha nchi 21 ikiwamo Tanzania, Cameroon, Jamhuri
ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Namibia, Sierra Leone,
Afrika ya Kusini, Togo na Zimbabwe.
Aidha, mbali
na nchi wanachama, zipo pia nchi waangalizi ambazo jiolojia ya nchi husika zina
uwezo wa kuzalisha madini hayo siku za usoni ambazo ni pamoja na Algeria,
Mauritania, Ivory Coast, Liberia, Mali na Mauritania.
Mwaka 2022
wakati Tanzania ikiwa mwenyekiti wa umoja huo iliwezesha kupitiwa kwa mifumo
kadhaa ya jumuiya hiyo ikiwemo Katiba, Kanuni na miongozo mbalimbali ambayo
yote ililengakuhakikisha nchi wanachama zinanufaika na rasilimali hizo.
Katika kikao
hicho nchi ya Sierra Leone ndiyo mwenyeji na ni Makamu Mwenyekiti. Kupitia
Mkutano huu, Sierra Leone itakuwa Mwenyekiti baada ya Zimbabwe kumaliza kipindi
chake. Kwa mujibu wa Katiba, mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la umoja huo
hudumu kwa kipindi cha miaka miwili.
Wataalam wa
Wizara ambao wamefuatana na Dkt. Kiruswa ni pamoja na mwakilishi wa Balozi nchini Nigeria, Allen
Kuzilwa, Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia masuala ya wachimbaji wadogo
Francis Mihayo na wataalam mhandisi Abeid Kidindi na Henry Shadolo.
0 Maoni