Bodi ya
Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imeagiza Menejimenti
ya Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa kubuni mazao mapya ya Utalii kwa
kushirikiana na jamii inayozunguka Hifadhi hiyo.
Akizungumza jana
wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Mradi wa REGROW
ndani na nje ya eneo la Hifadhi hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA
Jenerali (Mstaafu) George Waitara alisema,
“Niwapongeze
kwa Elimu mnayoitoa kwa jamii kuhusu Uhifadhi na Utalii, tunaenda vizuri
nisisitize kubuni mazao mapya ya Utalii kwa kushirikiana na jamii inayozunguka
Hifadhi”.
Naye, Mjumbe
wa Bodi ya Wadhamini - TANAPA Dkt. Robert Fyumagwa aliipongeza Menejimenti ya
Hifadhi hiyo kwa namna ambavyo imewekeza katika kutoa elimu ya Uhifadhi na
Utalii kwa wanajamii wanaozunguka Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa.
Naibu
Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa alisema
Shirika kupitia Hifadhi ya Taifa Milima Udzungwa imefanikiwa katika kuhifadhi
rasilimali misitu na wanyama wanaopatikana katika Hifadhi hiyo.
“TANAPA
kupitia Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa imeshuhudia ongezeko kubwa za
watalii pamoja na mapato lakini lengo la kuanzishwa Hifadhi ya Taifa Milima ya
Udzungwa ni kulinda Bioanuai na vyanzo vya maji na hilo lengo tumefanikiwa sana,”
alisema Mwishawa.
Awali, akitoa
taarifa ya utekelezaji wa miradi ya REGROW katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya
Udzungwa, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,
Dora Batiho ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Milima ya Udzungwa
alieleza kuwa hifadhi inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa miundombinu ya utalii
(Canopy Walkway) na kuongeza kwenye jamii zinazozunguka Hifadhi zimenufaika
kupitia Benki Hifadhi za Jamii "Community Conservation Bank” (COCOBA)
ambapo Jumla ya shillingi millioni 568 ilitolewa kama fedha ya kutekeleza
miradi ya vikundi 35 vilivyopo vijiji vya (Mang'ula B, Msufini na Msosa)
Vikundi ambavyo vina wanachama 590 huku Miradi iliyochaguliwa na vikundi ikiwa
ni pamoja na miradi ya kilimo (mpunga, miwa na nyanya), ufugaji (kuku wa mayai,
kuku wa nyama, bata, samaki na nyuki), mapambo, mashine za kusaga, na kukoboa
nafaka.
Mwenyekiti wa
Kijiji cha Msufini kilichopo Kilombero Bw. Nicodem Mwalongo alibainisha faida
zinazopatikana kupitia mradi wa REGROW na COCOBA ni pamoja na kuboreka kwa Hali
ya Uhifadhi wa mazingira, Kuimarika kwa mahusiano kati ya hifadhi na jamii
zinazozunguka hifadhi, Kuboresha makazi ya wanachama, Kuongeza mashamba na
kulima Kilimo cha Kisasa, pia wanachama wameweza kuanzisha biashara mpya kama
maduka na biashara ndogondogo, Mradi wa elimu bora kwa watoto 54 pamoja na
uhakika wa bima ya afya kwa wanachama wote wa COCOBA.
Na. Edmund
Salaho - Udzungwa



0 Maoni