Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa ameliambia bunge kuwa mradi wa uzalishaji umeme katika Bwawa la Julius
Nyerere (JNHPP) umekamilika na tayari megawati 2,115 zimeunganishwa kwenye
gridi ya taifa na kuongeza kiwango cha umeme kufikia megawati 4,031.7.
Mhe. Majaliwa amesema kwamba
kuanza kwa uzalishaji wa umeme katika mradi huo kumeongeza kiwango cha
upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuwa chachu ya kasi ya maendeleo ya
nchi.
“Hadi Machi 2025, jumla ya
megawati 2,115 zimeunganishwa kwenye gridi ya taifa na hivyo kuongeza kiwango
cha umeme katika gridi ya taifa kufikia megawati 4,031.7, alisema Mhe. Majaliwa.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa ameeleza hayo wakati akisoma Hotuba ya Bajeti ya Ofisi yake na Bunge 2025/26
leo Aprili 9, 20225, na kusema Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa mradi
wa uzalishaji umeme katika Bwawa la Julius Nyerere kwa gharama ya shilingi
trilioni 6.6.
Amesema kuwa katika kipindi
cha Novemba, 2020 hadi Februari, 2025, Serikali pia imeunganisha umeme katika
vijiji 4,071 kwa gharama ya shilingi bilioni 1,593 na hivyo kuwezesha vijiji
vyote 12,318 vya Tanzania Bara kuunganishwa na umeme.
Ameeleza kuwa hatua
inayofuata baada ya kukamilisha mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vyote, ni
kupeleka umeme kwenye vitongoji ambapo jumla ya vitongoji 33,657 kati ya
64,359, sawa na asilimia 52.3 vimeunganishwa na huduma ya umeme.
Mhe. Majaliwa amesema kwamba
usambazaji wa umeme katika vijiji na vitongoji utawezesha wananchi kushiriki
kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hususan zinazohitaji nishati ya umeme
zikiwemo kuchomelea vyuma, useremala, kuchakata nafaka na kuchenjua madini.
0 Maoni