Wizara ya Maliasili na
Utalii imeendelea kuongeza jitihada zaidi za kukabiliana na Wanyamapori wakali
na waharibifu hususani Fisi katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili
kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na usalama.
Akizungumzia jitihada hizo
Jijini Dodoma, Mkurugenzi Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi (SACC) Fidelis Kapalata, amesema Wizara kupitia Jeshi la
Uhifadhi tangu imeunda kikosi kazi maalum cha kupambana na Wanyamapori
wanaoleta usumbufu kwenye makazi ya watu, imesaidia kutatua changamoto hiyo
hususani Mkoani Simiyu.
SACC. Kapalata amesema kuwa,
katika kikosi kazi hicho chenye Askari wa Uhifadhi 27 kwa kushirikiana na
serikali za Halmashauri za Wilaya katika Mkoa huo pamoja na wananchi, wameweza
kudhibiti Fisi zaidi ya 25 ambao walikuwa kero kubwa kwa wananchi.
"Napenda kutoa shukrani
na pongezi kwa askari wetu waliopo uwandani, wananchi na Serikali za Wilaya
zote za Mkoa wa Simiyu, kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika kuwakabili
Wanyamapori hao waharibifu, niendele kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana
askari wetu katika zoezi hili, ili tuweze kufikia malengo yanayokusudiwa".
Amesema SACC. Kapalata.
Aidha, SACC. Kapalata
amesema kuwa hivi karibu kumeripotiwa uwepo na Fisi waharibifu katika Kambi ya
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, ambapo tayari
Wizara imeshachukuwa hatua ya kupeleka kikosi kazi cha askari wake ambao
wamesha weka kambi na kazi ya kuwasaka Fisi hao imeshaanza.
"Kuhusu taarifa ya
uwepo wa Fisi hatarishi katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Wilayani Kongwa,
tumesha peleka askari wetu na tayari wameshaanza kazi ya kuwasaka Fisi hao ni
imani yetu tutaitokomeza changamoto hiyo kwa mafanikio makubwa kama ilivyokuwa
katika Mkoa wa Simiyu," aliongeza SACC. Kapalata.
Ikumbukwe kuwa, uongozi wa
Wizara ya Maliasili na Utalii umeendelea kuunga mkono jitihata za Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha
wananchi wanaishi kwa usalama bila kubughudhiwa na Wanyamapori wakali na
waharibifu, kwa kuchukuwa hatua mbalimbali hususan za matumizi ya teknolojia ya
kisasa, kuunda kikosi kazi maalum kutoka kwa askari wa Taasisi zote zinazounda
Jeshi la Uhifadhi, kuongeza vitendwa kazi, kuelimisha umma, kushiriana na
wananchi pamoja na uongozi wa maeneo husika.
Na. Sixmund Begashe - Dodoma
0 Maoni