Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewasihi Mabalozi
kuwaunganisha Watanzania wanaoishi katika nchi wanazowakilisha (Diaspora) ili
waweze kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia uwekezaji mbalimbali.
Makamu wa Rais amesema hayo
wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Sweden
Mheshimiwa Balozi. Mobhare Matinyi pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji
Mheshimiwa Balozi. Hamad Khamis Hamad, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino
mkoani Dodoma leo tarehe 09 Aprili 2025.
Amesema ni muhimu kuwatambua
Watanzania hao kutokana na utaalamu, elimu au ufanyaji biashara na kuwahimiza
kuwekeza nchini pamoja na kusikiliza maoni na changamoto zao ili kuzifanyia
kazi. Amewataka Mabalozi kuwahimiza Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania
kufuata sheria na taratibu za Mataifa husika pamoja na kufanya uwekezaji katika
ngazi ya familia zao zilizopo nchini ikiwemo kuwasaidia ndugu zao kupata elimu
pamoja na ujenzi wa majengo ya makazi na biashara.
Pia, katika mazungumzo hayo
Makamu wa Rais amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuliwakilisha Taifa
kwenye nchi hizo. Amewaasa Mabalozi hao kuendeleza ushirikiano wa Tanzania na
Mataifa hayo ambao umekuwepo kwa muda mrefu.
Makamu wa Rais amewasisitiza
Mabalozi hao kuhakikisha wanakuwa na taarifa za msingi juu ya maendeleo ya
Taifa la Tanzania ili kuwa na uwakilishi mzuri katika maeneo yao hususani
katika kutekeleza diplomasia ya uchumi. Aidha amewahimiza kuhakikisha
wanatambua fursa zinazopatikana nchini ikiwemo rasilimali iki kuweza kuvutia
wawekezaji kutoka katika mataifa wanayokwenda kuwakilisha.
Halikadhalika amewasihi
kufahamu takwimu za msingi za Mataifa wanayokwenda kuiwakilisha Tanzania
ikiwemo fursa mbalimbali, maeneo muhimu ya ukuzaji wa uchumi pamoja na sekta
mbalimbali za mataifa hayo. Amesema ni muhimu kuhakikisha wanakuwa na
ushirikiano na watunga sera na viongozi wakuu wa sekta binafsi katika mataifa
hayo.
Amewaasa kufahamu vema
vipaumbele vya Taifa, mikakati mbalimbali pamoja na utekelezaji wake ikiwemo
Dira ya Taifa, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na mipango ya
maendeleo ya miaka mitano na mwaka mmoja mmoja.
Aidha, amesema ni muhimu
kuendelea kuitangaza lugha ya Kiswahili katika nchi hizo ikiwemo kutafuta fursa
ya ajira kwa walimu wa kufundisha lugha hiyo pamoja na ukalimani. Amewahimiza
kukuza biashara ya Tanzania na Mataifa hayo ikiwemo kutafuta masoko ya bidhaa
za Tanzania pamoja na kuwaunganisha watanzania na fursa mbalimbali za
kibiashara.
Makamu wa Rais amesema kwa
Mataifa yaliyoendelea kiteknolojia, ni vema kuhakikisha Tanzania inashirikiana
nayo ili kuweza kupata manufaa zaidi katika matumizi ya teknolojia kwenye sekta
mbalimbali ikiwemo kilimo na viwanda. Pia amewahimiza Mabalozi kutafuta fursa
za mafunzo kwa vijana na kusisitiza zaidi katika ushirikiano wa elimu ya
ufundi, utafiti na kujenga uwezo wa kimfumo.
Amewataka kutangaza vema
Taifa ili kuvutia zaidi watalii, kushirikiana katika masuala ya mazingira
ikiwemo udhibiti wa taka pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta ya afya
hususani ujenzi wa viwanda vya dawa.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
09 Aprili 2025
Ikulu –
Chamwino Dodoma.
0 Maoni