Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka watendaji wa sekta ya nishati
kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa
huduma bora kwa wananchi.
Pia, ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Wafanyakazi EWURA kwa
uandaaji wa Taarifa za Maendeleo ya Sekta ya Nishati kwa Mwaka 2023/24 kwa
kuwa zina umuhimu mkubwa kwa Serikali katika
kufanya maamuzi, kwani zinasaidia kuona mwenendo wa sekta ya nishati kwa kuonesha
hali ya sekta hiyo ya nishati,
mafanikio, changamoto na fursa zilizopo katika kuiendeleza.
Dkt. Biteko ameeleza hayo
leo Aprili 9, 2025 jijini Dodoma wakati aliposhiriki katika uzinduzi wa Taarifa
za hizo Maendeleo ya Sekta ya Nishati kwa Mwaka 2023/24.
“ Wananchi wapewe majibu ya
haraka na ya haki, taarifa hii imeonesha bado tuna kazi kubwa ya kufanya.
Tunachotaka ni Watanzania kupata huduma iliyo bora na hiyo itasaidia kutokuwa
na malalamiko ya upatikanaji wa huduma kutoka kwa wananchi,” amesema Dkt.
Biteko.
Amesema kuwa Serikali
inaendelea kujenga vyanzo vipya vya umeme na kuweka msukumo mkubwa katika
uwekezaji wake ili kukabiliana na hatari ya uhaba wa umeme inayoweza kutokea
zisipofanyika jitihada za makusudi na za haraka.
“Mahitaji ya umeme
yameongezeka hadi megawati 254 ambapo ni sawa na kujenga mradi mwingine kama wa
Kidatu, ifikapo mwaka 2030 mahitaji ya juu ya umeme yatakuwa megawati 4,878 na
mwaka 2025 mahitaji ya juu ya umeme yatafikia megawati 8,055 taarifa hii
inaonesha hatari kama hatutachukua hatua,” amebainisha Dkt. Biteko.
Kwa upande wa sekta ndogo ya
gesi asilia, Dkt. Biteko amesema kama
zilivyo sekta nyingine za nishati kwa mujibu wa Taarifa hiyo, imeonesha kuwepo
ongezeko la matumizi ya gesi asilia viwandani, majumbani na kwenye vyombo vya
usafiri. Aidha, vituo vya kujaza gesi iliyoshindiliwa kwenye magari (CNG)
vimeongezeka.
Kuhusu mafuta amesema taarifa hiyo
inaonesha kuimarika kwa upatikanaji wa mafuta nchini pamoja na jitihada
za kuhamasisha wawekezaji wa ndani kujenga vituo vya mafuta katika miji midogo
na vijijini ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa bidhaa hiyo. Aidha,
amezipongeza kampuni za mafuta kwa kushirikiana vizuri na Serikali.
Katika hatua nyingine, Dkt.
Biteko amesema pamoja na jitihada za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa
nishati ya uhakika ya umeme, mafuta na gesi asilia bado sekta inakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwepo mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa
mazingira, upungufu na uchakavu wa miundombinu.
Ametaja changamoto zingine
ni za rasilimali fedha kwa ajili ya uwekezaji na za maendeleo ya sayansi na
teknolojia. Hata hivyo, ili kuondokana na changamoto hizo amesema , Serikali
kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kuhakikisha inaboresha,
inaimarisha, inarahisisha na inawezesha upatikanaji wa nishati safi kwa
Watanzania wote.
“ Namshukuru sana na
kumpongeza Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa mchango
mkubwa katika kuimarisha sekta ya nishati. Chini ya uongozi wake, tumeshuhudia
maendeleo makubwa katika sekta hii ikiwemo ukamilishwaji wa miradi mikubwa ya
kimkakati na kielelezo ambayo imeongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini,
upatikanaji wa bidhaa za petroli, pamoja na ongezeko kubwa la matumizi ya gesi
asilia hususani kwenye magari,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Wizara ya Nishati, Mhe. Judith Kapinga “Naendelea kumpongeza Rais
Samia kwa kazi kubwa inayofanyika katika sekta ndogo ya nishati, na usimamizi
mzuri wa Dkt. Biteko unaowezesha kupata mafanikio yote haya,” ameeleza Mhe.
Kapinga.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi EWURA, Prof. Mark Mwandosya ameishukuru na kuipongeza Serikali kwa
uwekezaji mkubwa inaoendelea kuufanya katika sekta ya nishati.
“ Hii miradi mikubwa hasa ya
umeme mfano Bwala la Julius Nyerere inachukua muda mrefu hadi kukamilika kwake
hivyo ni kiashiria kwamba tuanze sasa kutekeleza miradi mingine ili baada ya
miaka kadhaa tusijekupata changamoto ya umeme,” amesema Prof. Mwandosya.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA), Dkt. James Andilile amesema
kuwa uzinduzi wa taarifa hizo ni takwa la kisheria na tayari wameshafanya hivyo
kwa upande wa sekta ya maji.
Amesema katika sekta ndogo
ya umeme hadi kufikia Juni 2023/2024 uzalishaji wa umeme ulikuwa megawati 2,411
na sasa umefikia megawati 4,032.
“Kutokana na kuongezeka kwa
uzalishaji wa umeme huduma imeimarika na sasa changamoto iliyokuwepo
imeondolewa. Kuhusu gharama za bei ya umeme kutokana na uwekezaji katika
miundombinu hali ya fedha TANESCO imeendelea kuimarika na mwaka wa tatu
mfululizo imetengeneza faida kutokana na usimamizi wa Serikali wa kuondokana na
mitambo ya kukodi ya kuzalisha umeme,” amesema Dkt. Ndugulile.
Ameongeza kuwa katika sekta
ya mafuta hadi kuishia Juni 2023/2024 vituo vya mafuta vilikuwa 2,361 sawa na
ongezeko la asilimia 10, kukiwa na vituo 480 vijijini sawa na ongezeko la
asilimia 12. Pia, kuhusu gesi asilia amesema
katika mwaka 2020/2023 vyombo vya moto vilivyokuwa vinatumia gesi asilia
vilikuwa 7,000 na kufikia Machi mwaka
huu vimefikia 15,000 ikiwa ni sawa na asilimia 49.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni