WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Watanzania wana wajibu
wa pamoja wa kuhakikisha urithi wa utamaduni wa Taifa unalindwa, unaenziwa na
kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema hatuwezi kuwa na Taifa bila kuwa na utamaduni unaolitambulisha
na kututofautisha na mataifa mengine. “Utamaduni ni utambulisho wetu halisi
kama Taifa. Utamaduni wa Taifa letu ndiyo unatufanya tutambuliwe kuwa sisi ni
Watanzania bila kujadili tofauti za makabila, jamii au sehemu tunazotoka.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 22, 2025)
alipofungua Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Utamaduni na Maendeleo ya Michezo
kilichofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere,
jijini Dar es Salaam.
“Kamwe tusikubali kukumbatia tamaduni zinazokwenda kinyume
na maadili na ustaarabu wetu. Tusikubali kuwa watumwa wa tamaduni za kigeni
ambazo zinadhalilisha utu wetu. Pamoja na umuhimu wa kujifunza mambo mazuri ya
tamaduni nyingine ni lazima kuchuja nini cha kuchukua na nini cha kuacha.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania
kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan inathamini sekta za utamaduni, sanaa na michezo kutokana na
umuhimu wake kwa ustawi wa Taifa, hivyo wananchi washirikiane kuwarithisha
watoto na vijana misingi ya utamaduni.
Aidha, Waziri Mkuu amesema pamoja na utambulisho wa jamii,
kupitia sekta za utamaduni, sanaa na
michezo, pia jamii inapata manufaa makubwa ikiwemo kuzalisha ajira kwa
mamilioni ya Watanzania na kukuza uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa sekta hizo pamoja na
kutumika kusukuma agenda mbalimbali za Kitaifa pia ni chanzo cha furaha,
burudani, kuelimisha, kuonya na kuhamasisha umma katika nyanja mbalimbali.
Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa
Paramagamba Kabudi ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuzipa kipaumbele sekta za utamaduni, Sanaa na michezo na
hivyo kuziwesha kuwa na mafanikio makubwa. “Michezo ina nguvu na ushawishi
mkubwa katika kuleta maendeleo na miongoni mwa michezo inayoongoza kuliletea
Taifa fedha nyingi za kigeni ni riadha.”
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Mchezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tabia Maulid Mwita amempongeza Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na
mageuzi makubwa aliyoyafanya katika sekta.
Awali, Naibu Waziri
wa Habari, Utamaduni, Hamisi Mwinjuma amesema kuwa ili kuendelea kuvutia
mageuzi ya kidijitall, Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -
TAMISEMI, imefanikisha uunganishaji wa Mfumo wa Wadau wa Sanaa (AMIS) na Mfumo
wa TAUSI. Ametolea mfano mapato ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
yameongezeka kwa asilimia 200 kutokana na kuunganishwa kwa mifumo hiyo ya
makusanyo.
Amesema kuwa hatua hiyo si tu imeimarisha usimamizi wa sekta
ya sanaa, bali pia imefungua ukurasa mpya wa uwazi, urahisi wa upatikanaji wa
huduma, na uboreshaji wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. “Kuanzia tarehe 26
Februari 2025, mifumo hii miwili inafanya kazi kwa pamoja, na sasa wadau katika
maeneo 15 ya biashara - ikijumuisha studio za muziki, picha, video, huduma za
burudani na ubunifu - wanaweza kupata vibali kwa njia moja ya haraka na ya wazi
zaidi.”
Naye, Katibu Mkuu
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema kuwa Kikao
kazi hicho ni cha kimkakati katika kuleta mabadiliko makubwa kwa sekta za
utamaduni, sanaa na michezo ikiwa ni pamoja na kurahisisha utekelezaji wa
maazimio ya vikao vilivyopita.
Amesema kuwa kupitia
vikao kazi vilivyopita, Wizara imewezesha kuanzishwa kwa Kitengo cha Utamaduni,
Sanaa na Michezo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa,Kujengewa uwezo kuhusu
matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa usajili wa vyama na vilabu vya michezo
nchini
“Kupitia vikao hivi, tumeweza kuongeza idadi ya wataalamu wa utamaduni kutoka 43 mwaka 2021 mpaka 123 mwaka 2025 na Maafisa Maendeleo ya Michezo kutoka 48 mwaka 2021 hadi Maafisa Maendeleo ya Michezo 139 mwaka 2025.”




0 Maoni