Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amewataka Watanzania kuishi kwa upendo na kushirikiana kwa maslahi
mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 61 ya
Muungano, ambapo amewahimiza Watanzania kukumbuka kuwa kuwa Baba wa Taifa
Hayati Mwl. Julius Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume waliunganisha
Tanganyika na Zanzibar katika misingi ya umoja, amani, ushirikiano na
kuheshimiana hivyo, muhimu kuendeleza misingi hiyo ili kuenzi Muungano.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 26, 2025 katika mkutano
wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Soko la Kilombero, Wilaya ya Arusha
Mjini, Mkoa wa Arusha.
“ Arusha mfanye kazi kwa kushirikiana, muijenge Arusha yenu
mkumbuke kwenye nafasi zetu za uongozi mjue kesho hamtakuwepo mtaondoka, kila
mahala ulipo acha alama njema itakayo kumbukwa na wengine. Sisi tuliopo leo
tutakumbukwa kwa lipi, iwe changamoto tunapokumbuka miaka 61 ya Muungano tujue
ni alama gani tutaacha kwa watoto wetu,” amesema Dk. Biteko.
Amesema katika kuelekea Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba 2025
Watanzania waishi kwa kuvumiliana na kuheshimiana na kuwa wamoja kwa kuchagua
viongozi wanaoweza kuwasilisha ajenda zao kwa wananchi.
“ Hicho ndicho kiwe kipimo na viongozi tusitumie tofauti
zetu kutafuta kura, usiende kanisani au msikitini kwako kutumia uhalali
watofauti zetu kutafuta kura asitokee yeyote kufanya hivyo tuuenzi Muungano na
Rais Samia ameapa kuulinda Muungano huu kwa wivu mkubwa,” amesema Dk. Biteko.
Dkt. Biteko amebainisha Watanzania wasiruhusu Taifa
kugawanyika kwa sababu yoyote ile wakumbuke kuwa kama hakuna amani hakuna
biashara wala maendeleo yanayoweza kufanyika.
Pamoja na hayo, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ndani
ya kipindi cha miaka minne, imetekeleza miradi mingi na kusimamia sera na
mikakati mbalimbali ili kuuletea maendeleo Mkoa wa Arusha huku akitaja baadhi
ya hatua hizo kuwa ni kuboresha miundombinu ya barabara, ambayo inaiunganisha
Arusha na mikoa na maeneo yote ya kimkakati. Kwa mfano, Barabara ya Arusha-
Namanga, ambayo inakwenda hadi Nairobi nchini Kenya.
Hatua nyingine ni kuweka Sera na Mipango mbalimbali ya
kuiendeleza Arusha kimkakati. Kwa mfano, kuwa mwenyeji wa Makao Makuu ya EAC
pamoja na Taasisi zake nyingine. Pamoja na kuiendeleza Arusha kuwa mwenyeji wa
Taasisi nyingi za Kimataifa kwa sasa na kwa kipindi cha baadaye. Kwa mfano Chuo cha ESAMI, Mahakama ya Afrika
ya Haki za Binadamu na Watu pamoja na Taasisi nyingine.
Fauka ya hayo Dkt. Biteko amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania
kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya umeme na kusema kuwa Serikali
itahakikisha inafikisha huduma ya umeme kwa wananchi wote.
Kuhusu nishati safi ya kupikia Dkt. Biteko amegawa mitungi 500 ya gesi kwa baba lishe na mama lishe kwa lengo la kuwapa hamasa wanachi ili kuondokana na matumizi ya nishati isiyo safi. Huku akiwataka kuwa mabalozi wema wa nishati hiyo kwa jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema katika
awamu ya kwanza Mkoa huo umepokea mitungi ya gesi 1,000 na majiko kwa ajili ya
kusambaza kwa mama na baba lishe mkoani humo.
Ameongeza kuwa Serikali ina mpango wa kuwawezesha
wafanyabiashara wadogo kwa kutumia Mfuko maalum wenye fedha shilingi bilioni 10
na wamemuomba Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,
Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima azindue Mfuko huo mkoani humo ili kutoa fursa pia ya
wafanyabiashara wa mkoa huo kunufaika.
Vilevile, amesema Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria
kuuletea maendeleo Mkoa huo kwa kutoa
fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi
sambamba na kuimarisha sekta ya utalii kwa kujenga barabara mpya ya bypass
yenye urefu wa km 70, reli ya kisasa kutoka Dar
es salaam hadi Tanga, bandari ya nchi kavu yenye uwezo wa kuhifadhi
magari 600.
Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Mrisho Gambo amemshukuru Rais
Samia kwa kuwapatia mradi mkubwa wa maji na kuwaomba AUWSA kusaidia kuboresha
ufungaji wa mita za maji kwa wananchi hasa zilizo mbali na makazi yao.
Aidha, amesema katika upande wa sekondari Rais Samia
amejenga shule mpya za sekondari tano na shule mpya za msingi. Pia ameomba
wanafunzi wanaofaulu wapangiwe shule hizo kwa kuzingatia maeneo wanayoishi.
“Tunamshukuru pia Rais Samia kwa kutujengea uwanja wa mpira
unaogharimu shilingi bilioni 286, barabara za lami na viwanja vipya vitano
vidogo vya michezo,” amesema Mhe. Gambo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya MajiSafi
na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha – AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba akitoa
taarifa ya mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha amesema kuwa mradi
huo umegharimu shilingi bilioni 520 ikiwa ni fedha za Serikali na mkopo kutoka
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa sasa unazalisha maji zaidi ya lita
milioni 200 ambapo mahitaji ni lita milioni 139.
Licha ya mradi huo kufanikiwa kupita lengo la upatikanaji wa
huduma ya maji kwa wananchi kama lilivyoelezwa kwenye Ilani ya Chama cha
Mapinduzi, Mhandisi Rujomba ametaja
faida za mradi huo kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya wateja hadi kufikia 100,000,
kuongezeka kwa uwezo wa kutibu maji taka na kununua mtambo wa kupima utendaji
kazi wa dira za maji.
“Kupitia mradi huu wakandarasi wameweza kununua vifaa kwenye
soko la ndani vya gharama ya shilingi bilioni 150 hivyo umesaidia kukuza
uchumi, pia tumepata ajira a watu 2,000 ikiwemo wanawake , tumeweza kujenga
ofisi za kanda ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi, na tuna uwezo wa
kuhifadhi maji zaidi ya nane hata kama kuna matengenezo ,” amesema Mhandisi
Rujomba.
Naye, Meneja Mradi Upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha
Njiro kilichoongezwa transforma yenye uwezo wa MVA 90 kufanya kituo kuwa na
uwezo wa MVA 210, Mhandisi Japhari Msuya
ametaja faida za kukamilika kwa mradi huo kuwa ni kutaimarisha upatikanaji wa
umeme kwenye mikoa ya kanda ya kaskazini na kuendelea kufungua fursa za
kiuchumi kwenye mikoa ya kanda ya kaskazini na kuimarisha sekta ya utalii,
viwanda na biashara.
Akiwasilisha salamu za Muungano, kutoka Ofisi ya Makamu wa
Rais, Muungano na Mazingira, Mratibu wa Muungano, Bw. Tumsifu Mwasamale amesema
kuwa kwa mwaka huu 2025 ilielekezwa kuwa sherehe hizo zifanyike kwa wananchi na
hivyo kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa uratibu na maandalizi mazuri ya
sherehe hizo za Muungano.
Dkt. Biteko amehitimisha ziara yake siku tano mkoani humo
kwa kutembelea Wilaya za Monduli, Longido, Aumeru na Arusha Mjini ambako
amekagua na kuzindua miradi kutembelea, kukagua na kuzindua miradi ya
maendeleo, kupanda miti miti ya kumbukumbu na kuhutubia wananchi mikutano ya hadhara
ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
0 Maoni