Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa Watanzania kuendeleza fikra za Mwl.
Nyerere kwa kuwekeza katika sekta za elimu, kilimo, viwanda, teknolojia na
biashara ndogo ndogo zinazotegemewa na wananchi wengi ili kukuza uchumi
jumuishi.
Aidha, Serikali na sekta
binafsi zinapaswa kushirikiana ili kuhakikisha uwekezaji unaleta tija kwa
wananchi wa kawaida.
Dkt. Biteko amesema hayo leo
Aprili 11, 2025 jijini Dar es salaam wakati aliposhiriki katika Kongamano la
Kumbukizi ya Kuzaliwa Kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Amesema Kongamano hilo lenye
mada inayosema Maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika
Elimu, Uwekezaji na Ujenzi wa Taifa lenye Amani kwa Maendeleo ya Watu ni fursa
ya kufanya tafakuri kwa baadhi ya mambo ambayo Baba wa Taifa aliyaamini,
aliyaishi na anaendelea kukumbukwa nayo.
“Maono ya Mwalimu kuhusu
uwekezaji kwa maendeleo yalilenga kuimarisha uchumi wa Taifa kwa misingi ya
usawa na uwajibikaji wa pamoja.
Alisisitiza kuwa uwekezaji
lazima uwalenge wananchi na kuhakikisha kwamba rasilimali za Taifa zinatumika
kwa manufaa ya wote. Alipinga mifumo ya kiuchumi inayozalisha matabaka na
ukosefu wa haki, huku akihimiza ujamaa na kujitegemea,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Mwl. Nyerere
alitamani kuona elimu inampa mwanafunzi maarifa ya kumwezesha kuchangia
maendeleo ya jamii yake na sio ya kumtenga na mazingira yake. Aidha, jamii
inapaswa kujiuliza ikiwa sasa elimu inawajenga Watanzania kuwa raia wenye uwezo
wa kutatua matatizo yao na kuchangia maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.
Amebainisha kuwa katika
dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa wa kiteknolojia na kiuchumi, ni muhimu
kuwekeza katika elimu inayozingatia maendeleo ya sayansi, teknolojia, ubunifu
na stadi za maisha ili kujiletea maendeleo ya kweli.
Akizungumzia umuhimu wa
amani, Dkt. Biteko amesema kuwa hakuna maendeleo yanayowezekana bila amani na
mshikamano wa kitaifa.
“Kupitia misingi ya utaifa
na umoja, aliweza kujenga Taifa lenye mshikamano thabiti licha ya tofauti za
kikabila, kidini, na kijamii. Leo taifa letu linanufaika na amani, umoja na
upendo wa kindugu ambavyo Baba wa Taifa alivijenga kwa juhudi kubwa,”amesema
Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa Bodi wa Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere na Makamu Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara, Mhe. Stephen Wasira ameelezea sifa na
jitihada mbalimbali alizofanya Mwalimu Nyerere wakati wa harakati za kupigania
uhuru wa Tanganyika kutoka kwa wakoloni.
“Aliunganisha nchi zetu kwa
sababu aliamini Afrika lazima iwe moja, aliaamini katika umoja, leo tunakumbuka
miaka 103 ya kuzaliwa kwake, kiongozi ambaye aliongoza Taifa hili kwa miaka
24,” amesema Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo.
Naye, Mkuu wa Chuo cha
Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere, Prof. Haruni Mapesa amesema kuwa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere hakuwa kiongozi wa kitaifa pekee bali kimataifa na aliyeweka
misingi muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Amesema Chuo hicho
kilianzishwa na Mwl. Nyerere na baadaye kuwa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere na
kina dira ya kuwa kitovu cha utoaji wa elimu bora na kuendeleza amani nchini.
Amebainisha kuwa Chuo hicho
cha Mwl. Nyerere kimekuwa na desturi ya kufanya makongamano hayo kila mwaka kwa
lengo kuenzi, kuzungumza na kupigia debe mawazo na falsafa na misingi yake
katika Taifa.
“ Mwalimu aliamini kuwa elimu ni nyenzo kuu ya uongozi na
alisisitiza elimu ya kujitegemea. Leo tunapomuenzi tujiulize je tunazifuata falsafa
zake za elimu kuwaandaa vijana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa au kuwa watafuta
ajira,” amesema Prof. Haruni.
Pamoja na hayo, ametaja
baadhi ya mafanikio yaliyopatikana chuoni hapo katika kipindi cha uongozi wa
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ni
maboresho makubwa ya miundombinu ya kujifunza na kufundishia.
Licha ya maboresho hayo, Prof. Mapesa amesema
Chuo hicho kinaendelea na ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maktaba ya
kisasa itakayo hifadhi machapisho mbalimbali yenye tija kwa Taifa.
Ameongeza kuwa Chuo hicho
kinatimiza lengo la Mwl. Nyerere la kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata
elimu ya sayansi ya jamii, uzalendo na uongozi katika maeneo mbalimbali
waliyopo, na kuwa sasa wana wahadhiri wenye shahada ya uzamivu wafikao 59 na
wengine wakiendelea na masomo na ndani ya kipindi cha miaka miwili watakuwa na
wahadhiri wenye shahada ya uzamivu 100.
Aidha, kupitia Kongamano la
mwaka huu kumekuwa na mashindano ya insha kwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari juu ya Mchango wa Mwalimu Nyerere kuhusu Elimu ya Kujitegemea katika
Maendeleo ya Taifa.
Lengo la mashindano hayo ni
kuwafanya vijana kuendelea kujifunza kuhusu falsafa za Baba wa Taifa na
kuzitumia ambapo Dkt. Biteko alikabidhi zawadi kwa washindi pamoja na yeye
kutunukiwa tuzo na Chuo hicho.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni