Ofisi ya Msajili wa Hazina
imefanya kikao na Wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Shirika la Hifadhi za Taifa
Tanzania (TANAPA) leo, Aprili 10, 2025, katika ukumbi wa mikutano uliopo Shule
ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere (Mwalimu Julius Nyerere Leadership
School), Kibaha, Pwani. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti, Peter Maungo,
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Mashirika ya Kibiashara ya Umma.
Kikao hicho kilikuwa na
dhima ya kujadili na kupitisha bajeti mpya ya TANAPA kwa mwaka 2025/2026,
ambayo kipaumbele chake ni kuongeza fursa za uwekezaji, kuanzisha mazao mapya
ya utalii, kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha ulinzi mkakati kwa
kutumia teknolojia, shughuli za uhifadhi na tafiti, pamoja na kuongeza fursa za
ajira kwa kuzingatia miongozo ya shirika la ubora wa kimataifa (ISO). Pia,
bajeti hiyo inalenga kudhibiti mimea vamizi na wanyamapori wakali na
waharibifu, kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi,
na kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.
Kamati ya Bajeti ya Shirika
iliongozwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Juma Nassoro Kuji, ambapo
aliambatana na wataalamu waandamizi kutoka idara mbalimbali za Shirika hilo.
Katika kikao hicho, Kamishna Kuji alieleza kwa kina mwelekeo wa kimkakati wa
Shirika katika mwaka wa fedha 2025/2026, akisisitiza umuhimu wa kuongeza
ufanisi katika matumizi ya rasilimali, kuimarisha mifumo ya usimamizi, na
kukuza ushirikiano kati ya TANAPA na wadau mbalimbali wa
uhifadhi na utalii.
0 Maoni