Bodi ya Kampuni ya Misitu
(MCL), kampuni tanzu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imeanza
rasmi kazi zake na kupewa matarajio tisa ya utekelezaji kutoka kwa Bodi ya
Ushauri ya TFS.
Akizungumza katika kikao cha
kwanza cha utambulisho wa bodi hiyo, kilichofanyika leo mkoani Morogoro,
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TFS, Meja Jenerali Dkt. Mbaraka Mkeremy,
alisema Kampuni ya Misitu ilianzishwa kama mkakati wa kibiashara wa TFS kwa
lengo la kuanzisha na kuendeleza miradi ya kibiashara inayotumia rasilimali za
misitu na nyuki.
“Lengo kuu la miradi hii ni
kuongeza mapato ya Wakala na kupanua biashara zinazotegemea rasilimali za misitu
na nyuki,” alisema Meja Jenerali Mkeremy.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo
itakuwa na jukumu la kuandaa mapendekezo ya miradi, kushughulikia mipango ya
uwekezaji, na kupunguza utegemezi wa Wakala kwa Serikali.
“Hivyo kipimo chetu kitakuwa
ni kiwango cha mapato kinachoongezeka kwa taasisi kutokana na kazi za kampuni,”
alisisitiza Mkeremy.
Matarajio tisa yaliyotajwa
na Bodi ya Ushauri ya TFS kwa Kampuni ya Misitu ni pamoja na kuimarisha
utendaji wa kibiashara, kuongeza thamani ya mazao ya misitu, kuongeza mapato,
na kuboresha huduma na bidhaa.
Mengine ni kukuza ubunifu na
matumizi ya teknolojia, kujenga ushirikiano na wadau mbalimbali, kusimamia
sheria na taratibu, kukuza ujuzi na mafunzo kwa watumishi, pamoja na kuhimiza
weledi na uaminifu katika utendaji wa kazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti
wa Bodi ya Kampuni ya Misitu, Ndugu Fortunatus Mhambe, alishukuru kwa maelekezo
yaliyotolewa na Bodi ya Ushauri ya TFS, na kwa niaba ya wajumbe wenzake
aliahidi kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo na bidii ili kufikia malengo
yaliyowekwa.
Wajumbe wengine wa bodi hiyo
ni Neema Mbise, Peter Mwakosya, Prof. Yonika Nganga, na Chelestino Balama.
Katibu wa Bodi ni Bi. Salome Rwiza.
0 Maoni