Kwa mara ya kwanza wataalam wazawa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila wamefanya upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye pafu la mgonjwa kwa njia ya matundu madogo (Thoracoscopy).
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara
ya Upasuaji MNH-Mloganzila Dkt. Eric Muhumba huduma hiyo ya ubingwa bobezi
imefanywa na wataalam wa Muhimbili Mloganzila kwa kushirikiana na Muhimbili
Upanga ambako huduma hii ilianza kutolewa.
Dkt. Muhumba ameongeza kuwa
manufaa ya huduma hiyo ni pamoja na mgonjwa kupunguza maumivu wakati na baada ya upasuaji,
kupunguza muda wa kukaa hospitalini hususani wodi ya uangalizi maalum, mgonjwa
kutokuwa na kidonda kikubwa na makovu makubwa.
“Tumekuwa tunatoa huduma
hizi hapo awali kwa kufungua kifua na kutoa uvimbe lakini kwa mara ya kwanza
tumefanikiwa kutumia matundu madogo na mgonjwa anaendelea vizuri, wataalam
tunaendelea kumfuatilia kwa karibu,” amesema Dkt. Muhumba.
Dkt. Muhumba amebainisha
kuwa kufanikiwa kwa huduma za ubingwa bobezi zikiwemo za matundu madogo
kumetokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya afya ikiwemo
kusomesha wataalam, uwepo wa vifaa tiba vya kisasa vya kutolea huduma na
mazingira wezeshi na rafiki ya kufanyia kazi.
Hospitali ya Taifa
Muhimbili-Mloganzila imejipambanua kwa kuanzisha huduma nyingi za ubingwa
bobezi na kuwapunguzia Watanzania usumbufu na gharama kwenda nje ya nchi
kutafuta huduma hizo na kuwavutia watu mbalimbali kutoka mataifa jirani
kunufaika na huduma zilizopo nchini.
0 Maoni