JUMLA ya leseni 1356 za uchimbaji madini zimetolewa katika halmashauri tatu za
Mkoa wa Kimadini Kahama ambazo ni Ushetu, Msalala na Kahama huku wazawa na
wawekezaji kutoka nje wakitakiwa kuchangamkia fursa zilizopo mkoani humo.
Akizungumza Afisa Madini Mkazi wa Kahama Leons Welengeile amesema, leseni za utafutaji madini zipo
jumla 77 ambazo zinahusisha utafutaji wa dhahabu kwa asilimia kubwa, leseni
kubwa za uchimbaji zipo katika maeneo mawili ambayo ni migodi ya Bulyanhulu na
Buzwagi.
“Kwa sasa shughuli zinafanyika katika mgodi wa Bulyanhulu na
mgodi wa Buzwagi upo katika hatua za
ufungaji mgodi,”amesema Leons.
Amesema, mbali na hatua za ufungaji mgodi pia katika eneo la
mgodi wa Buzwagi yapo maeneo yaliyotengwa maalum (Special Economic Zone) kwa
ajili ya shughuli za uwekezaji wa viwanda na yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili
ya taasisi za elimu.
“Katika eneo hilo kwa sasa takribani kilomita za mraba 13
zimetengwa na kuwa eneo maalum la uwekezaji ambapo kuna shughuli mbalimbali
zinaendelea ikiwemo uwekezaji katika utengenezaji wa vifaa na vipuri mbalimbali
vinavyotumika migodini, viwanda vya utengenezaji baruti na viwanda vya
uongezaji thamani madini,”amesema Leons na kuongeza.
“Pia kuna maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji wa
taasisi za elimu hususan elimu ya ufundi ambazo zimelenga kukuza uelewa na
utaalam kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya Wilaya ya Kahama wa shughuli
mbalimbali za migodini.
“Mbali na hivyo, tunasimamia leseni saba za uchimbaji wa
kati na mbili zipo katika hatua ya ufungaji mgodi, lakini pia kuna leseni nne
zipo kwenye hatua ya uendelezaji na moja ipo kwenye hatua ya uchimbaji,” amesema.
Leons amesema pia, hadi mwezi Februari 2025 wametoa jumla ya leseni 1270 za uchimbaji mdogo
na asilimia 40 ya leseni hizo ndio zimeendelezwa na asilimia 60 zipo kwenye
hatua mbalimbali za utafiti.
Aidha, amesema kuna fursa nyingi katika Mkoa wa Kimadini
Kahama ambazo ni fursa za biashara ya
madini ambapo lipo soko moja na vituo
vitano vya ununuzi wa madini.
Pia amesema kuna fursa ya ujenzi wa mitambo ya uchenjuaji wa madini ambayo kwa sasa ni
michache kwa maana wachimbaji wamehamasika kuachana na matumizi ya zebaki
kwenda kwenye matumizi ya kuchenjua kupitia mitambo ya CIP.
Amesema, katika Mkoa wa Kimadini Kahama, wana miradi mitatu
ya uendelezaji wachimbaji wadogo kwa
njia ya Mikataba ya Msaada wa Kiufundi
‘technical support agreement’, ambayo ni Shangaza, LHT na Super Mabomu.
“Awali shughuli za uzalishaji katika maeneo hayo zilikuwa ni chache ambapo wastani ilikuwa kilo moja au mbili za madini ya dhahabu ndio zilikuwa zikizalishwa, lakini kutokana na uwekezaji uliofanywa kwa njia ya Mkataba wa Msaada wa Kiufundi, tumeshuhudia maeneo hayo kwa sasa uzalishaji umeongezeka hadi kufikia wastani wa kilo tano za madini ya dhahabu kwa mwenzi,” amesema.
0 Maoni