WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amezitaka jumuiya za wafanyabiashara nchini
kuendelea kuwa na imani na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani amedhamiria
kutatua changamoto zinazohusu masuala ya kodi.
Amesema Rais
Dkt. Samia anajali changamoto za wafanyabiashara na ndio maana ameunda timu
mbalimbali kwa ajili ya kufanya mapitio ya kero za wafanyabiashara wafanye kazi
zao kwa uhuru.
Mheshimiwa
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Jumapili 23 Machi 2025) alipokuwa akijibu hoja
zilizotolewa na Mwakilishi wa wafanyabiashara wa Halmashauri ya Makambako
aliposimama na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo.
"Nataka
niwatoe Mashaka Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan baada ya mapendekezo yenu
wafanyabiashara yale kumi na tano, kufuatia mkutano na wafanyabiashara Kariakoo
ameunda tume inayofanya mapitio ya mfumo wa kodi Tanzania na inaendelea
kuzunguka nchi nzima kufanya kazi hiyo."
Aidha,
amempongeza Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kusimamia vyema
ukusanyaji wa mapato nchini sambamba na kuchukua hatua kwa watendaji wa Mamlaka
hiyo ambao wanaenda kinyume na maadili yao ya kazi.
Pia amemtaka
kamishna huyo kuendelea kuboresha programu za utoaji wa elimu kwa mlipa kodi,
ili kuondoa changamoto zinazowakabili wafanya biashara kuhusu masuala ya kodi.
"Serikali
hii inamtaka kila mtanzania ajue umuhimu wa kulipa kodi na tunajua kuwa sasa
watanzania wengi wanajua umuhimu wa kulipa kodi."
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametembelea kiwanda cha uchakataji zao la
parachichi cha Avo Afrika, kilichopo Mkoani Njombe.
Akizungumza
na wafanyakazi na baadhi ya wananchi wanaouza bidhaa zao katika kiwanda hicho,
Mheshimiwa majaliwa ametoa wito kwa wakulima wa zao la parachichi kuendelea
kulima zao hilo kwani sasa zao hilo lina soko la uhakika.
"Nataka
niwaambie sasa hali imebadilika parachichi ni biashara tosha, kama unataka
utajiri lima parachichi, ukilima leo una uhakika wa mahali pa kuuza kwa sababu
sasa wawekezaji wa uhakika wapo."


0 Maoni