Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi imetangaza kuongeza siku mbili zaidi za zoezi la uboreshaji
wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Dar es Salaam ambapo sasa zoezi hilo
litamalizika Machi 25, 2025.
Hatua hiyo
imetangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa
Rufani Jacobs Mwambegele leo Machi 23, 2025 kufuatia mwitikio mkubwa wa
wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao kujitokeza kwa wingi katika zoezi la
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulioanza Machi 17 na uliotarajiwa
kumalizika leo Machi 23 mwaka huu.
“Hivyo basi,
napenda kuwatangazia wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa, Tume
imeongeza siku mbili za uboreshaji wa Daftari kwa tarehe 24 na 25 Machi, 2025
na zoezi litakamilika tarehe 25 Machi, 2025 saa 12:00 jioni,” amesema Jaji
Mwambegele.
Aidha, Jaji
Mwambegele amefafanua kuwa baada ya siku hizo mbili Tume haitaongeza muda
zaidi.
Amesema
wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kujitokeza
kujiandikisha na kuboresha taarifa zao tangu siku ya kwanza ya zoezi hilo Machi
17, 2025 ambapo Tume iliongeza mashine za BVR pamoja na watumishi.
“Kutokana na
mwitikio mkubwa Tume ilichukua hatua za kuongeza mashine za BVR kits pamoja na
watumishi katika maeneo yote yaliyoonekana kuwa na watu wengi na hatua hii
imewezesha zoezi kuendelea kwa utulivu katika maeneo yote,” amesema Jaji
Mwambegele.
Alisema baada
ya kuongeza mashine za BVR na watumishi katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa na
changamoto ya watu wengi iliwezesha kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi na
kupunguza kwa kiasi kikubwa misongamano kwenye baadhi ya maeneo.
Jaji
Mwambegele amesema Tume inawapongeza wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kwa
kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa mara ya kwanza, kuboresha au kuhamisha
taarifa zao na kupata kadi mpya kwa wale ambao kadi zao zimepotea au
zimeharibika.
Katika hatua
nyingine Jaji Mwambegele alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi wa Mkoa wa
Dar es Salaam kuwa zoezi hilo halihusishi ubadilishaji wa kadi zilizotolewa
tangu 2015.
“Napenda
kuwakumbusha kuwa zoezi hili halihusishi ubadilishaji wa kadi za mpiga kura
zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 kwa kuwa kadi hizo ni halali na zitaendelea
kutumika kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge
na Madiwani,” alisema Jaji Mwambegele.
Ameongeza
“Hivyo, wananchi wote ambao kadi zao hazijaharibika au kupotea, hawajahama
kutoka kata au halmashauri hawahusiki na zoezi hili”.
Aidha, Jaji
Mwambegele ameonya kuwa kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa kisheria na
anayefanya hivyo akitiwa hatiani anaweza kufungwa jela, kutozwa faini au vyote
kwa pamoja. Kosa hilo ni kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 114(1) cha
Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024.
“Mtu yeyote
akithibitika amejiandikisha zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa na akitiwa
hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja
(100,000/=) na isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) au kutumikia kifungo
kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au
vyote kwa pamoja, kulipa faini na kifungo gerezani,” amesema.
Jaji
Mwambegele ametoa wito kwa wadau wote wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na wananchi
kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa Tume na kuhakikisha kuwa wanaokwenda
kujiandikisha na kuboresha taarifa zao vituoni ni wale tu ambao wanastahili
kufanya hivyo.
Tume
imeshakamilisha uboreshaji wa Daftari katika Mikoa 30. Kwa mujibu wa ratiba,
ambapo sasa uboreshaji upo katika mzunguko wa 13 ambao ni mzunguko wa mwisho wa
uboreshaji wa Daftari kwa awamu ya kwanza. Mzunguko huu unahusisha Mkoa wa Dar
es Salaam pekee.

0 Maoni