Imeelezwa
kuwa Sekta ya Madini nchini Tanzania inaendelea kuwa mhimili wa uchumi wa
Taifa, na kukua kwa kasi kutokana na mikakati thabiti ya Serikali kupitia
Wizara ya Madini yaliyopelekea kuongezeka kwa ufanisi na mchango wa Sekta
katika uchumi wa taifa kwa ujumla.
Hayo
yamebainishwa leo Machi 23, 2025 na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven
Kiruswa, wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini
kilichofanyika katika Ukumbi wa Corridor Spring Hotel jijini Arusha.
Dkt. Kiruswa
amefafanua kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana yametokana na mikakati
madhubuti inayotekelezwa na Wizara ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea
kuchangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa, huku Serikali ikiwekeza nguvu
kubwa katika kuimarisha ukuaji wake na kuhakikisha madini yanazalisha faida
zaidi kwa wananchi.
Amesema
kuwa, Serikali imejipanga kuhakikisha
Sekta ya Madini inakuwa na matokeo chanya kupitia maono ya Vision 2030: Madini
ni Maisha na Utajiri, mpango unaolenga
kuendeleza Sekta kwa kuongeza utafiti wa kina wa rasilimali madini, kuwezesha
wachimbaji wadogo, wa kati, na wakubwa, pamoja na kuhakikisha usimamizi bora wa
rasilimali hizi unaleta tija kwa Taifa.
Fursa kwa Vijana Kupitia Mining for
Better Tomorrow (MBT)
Ili
kuhakikisha Watanzania, hususan vijana, wananufaika zaidi na sekta ya madini,
Wizara imeanzisha mpango wa Mining for Better Tomorrow (MBT). Mpango huo
utawapa vijana nafasi za ajira, mafunzo maalum ya utafutaji na uchimbaji wa
madini, pamoja na kuwapatia vifaa vya kisasa vya uchimbaji.
“Vijana ndio
nguvu kazi ya Taifa, na kupitia mpango huu, tutahakikisha wanapata nafasi ya
kushiriki moja kwa moja katika sekta ya madini, siyo tu kama wafanyakazi, bali
pia kama wajasiriamali na wawekezaji wa baadaye,” amesisitiza Dkt. Kiruswa.
Kuimarishwa kwa Utafiti wa Madini
Nchini
Dkt. Kiruswa
amefafanua kuwa, ili kuhakikisha madini yanachangia zaidi katika uchumi, Wizara
imejipanga kuongeza utafiti wa kina wa madini kutoka asilimia 16 ya sasa hadi
kufikia asilimia 50 ya eneo lote la nchi ifikapo mwaka 2030. “Tunataka kubaini
maeneo yote yenye rasilimali madini kwa usahihi zaidi, ili kuwezesha wachimbaji
wadogo, wa kati, na wakubwa kufanya kazi kwa uhakika badala ya kubahatisha,”
amefafanua Dkt. Kiruswa.
Kwa hatua
hiyo, wachimbaji wadogo wataweza kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi, huku
Serikali ikipata mapato ya kutosha kwa ajili ya kuimarisha sekta nyingine
muhimu za kijamii kama afya, elimu, na miundombinu.
Wito kwa Wafanyakazi wa Sekta ya
Madini
Dkt. Kiruswa
amewataka wadau wote wa sekta ya madini kushirikiana na Serikali katika
kuboresha na kuendeleza sekta hii kwa manufaa ya wote. “Michango yenu ni muhimu
sana katika kuhakikisha tunatimiza malengo tuliyojiwekea kwa mwaka 2024/2025 na
pia katika kupanga mipango ya 2025/2026 kwa ufanisi zaidi,” amehimiza Dkt.
Kiruswa.
Mchango wa Madini Katika Uchumi Wazidi
Kupaa
Kwa upande
wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema kuwa, kwa mujibu
wa takwimu za Wizara, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa
umeongezeka hadi kufikia asilimia 9.0 mwaka 2023, huku kasi ya ukuaji ikifikia
asilimia 11.3 katika kipindi hicho. Hatua hiyo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa
na miaka ya nyuma, ambapo Sekta hii ilikuwa ikichangia kwa kiwango cha chini
zaidi.
Mbibo
amesisitiza kuwa mbali na mchango huo, mapato ya Serikali kutokana na maduhuli
yatokanayo na shughuli za madini yameendelea kuimarika huku akitolea mfano
kuwa, katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025, makusanyo yamefikia
shilingi bilioni 690.76, ongezeko la asilimia 42.04 ikilinganishwa na shilingi
bilioni 486.30 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Mauzo ya Madini Nje ya Nchi Yaongezeka
Aidha, Mbibo
ameongeza kuwa, thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi pia imeongezeka kwa
kasi, ikifikia dola za Marekani milioni 3,551.4 mwaka 2023, kutoka dola milioni
3,395.3 mwaka 2022. Ongezeko hilo la asilimia 4.6 linaonesha jinsi sekta hii
inavyoendelea kuwa tegemeo la mapato ya kigeni kwa Tanzania. Kwa sasa, madini
yanachangia asilimia 56.2 ya mauzo yote ya bidhaa zisizo za asili nje ya nchi,
jambo linaloifanya sekta hii kuwa mojawapo ya sekta zenye mchango mkubwa katika
uchumi wa Taifa.
Mafanikio Mengine Makubwa Katika Sekta
ya Madini
Naibu katibu
Mkuu Mbibo ameongeza kuwa, mbali na ongezeko la mapato na uwekezaji, Wizara ya
Madini imefanikiwa kutekeleza miradi mingine muhimu, ikiwa ni pamoja na:
Ununuzi wa
mitambo 10 ya uchorongaji (rigs) kwa ajili ya kuwezesha wachimbaji wadogo kupata
madini kwa urahisi na kwa teknolojia ya kisasa.
Utoaji wa
leseni kubwa ya uchimbaji wa madini ya kinywe (SML) kwa Kampuni ya EcoGraf
Limited, inayofanya kazi katika eneo la Epanko, Wilaya ya Mahenge – Morogoro.
Pamoja na
kukamilika kwa utafiti maalumu na kuchora ramani ya jiolojia ya visiwa vya
Zanzibar (Unguja na Pemba) ili kubaini fursa zaidi za madini
katika eneo hilo.
0 Maoni