Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya
Madini, imekutana na wadau wa madini ikiwemo Wathaminishaji wa Madini,
Wachimbaji Wadogo na Wanunuzi ili kupanga bei elekezi ya madini ya vito.
Akizungumza jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara
ya Madini, Venance Kasiki amesema lengo la kukutana na wadau hao ni kufanya
tathmini na kupanga bei mpya ya madini ya vito ambayo itatumika katika kipindi
cha miezi mitatu na kuhakikisha biashara ya vito inakwenda vizuri.
“FEMATA ni mzalishaji
wa madini, CHAMMATA na TAMIDA ni
wanunuzi wa madini ya vito, tumekutana ili kutengeneza bei elekezi, ambayo
itatumika kwa kipindi cha miezi mitatu, ili pande zote ziweze kunufaika....;
“Kikao kimeenda vizuri, bei zilizowekwa ni rafiki, zitanufaisha pande zote kwa
maana ya wachimbaji, wanunuzi na serikali itapata stahiki zake ikiwemo Mrabaha
na Ada ya Ukaguzi,”amesema Kasiki na
kuongeza.
“Bei zilizopendekezwa
ni za wazi na zitapatikana kwenye mitandao na Tovuti ya Tume ya Madini, hivyo
nawasihi wadau kupitia tovuti ya Tume ya Madini na ofisi za Afisa Madini
wakazi ili kujua bei elekezi,” amesisitiza.
Aidha, Kasiki amesema pia wamebaini changamoto mbali mbali
wanazokumbana nazo wathaminishaji madini na kwamba watakuwa wanakutana nao kila
robo ya mwaka lengo likiwa ni kutafuta suluhu ya changamoto hizo na
kubadilishana uzoefu kutokana na mabadiliko ya teknolojia duniani katika tasnia
ya uthaminishaji madini ili waende na wakati.
Naye mwakilishi kutoka Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa
Madini (FEMATA) Kalebi Gunda akizungumza kuhusiana na bei elekezi amesema ni
rafiki kwa wachimbaji.
“Kikao kimeenda vizuri hakuna atakayelalamika na kila mmoja
atapata manufaa kwa upande wake, wachimbaji watanufaika, wanunuzi watanufaika
na serikali nayo itapata stahiki yake ya mapaato kupitia Mrabaha na halmashauri
itapata tozo yake ya ‘service levy,” amesema Gunda.
Vyama vilivyoshiriki kikao hicho ni Chama cha Wachimbaji Madini Wanawake (TAWOMA), Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) na Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA).
0 Maoni