Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameendelea kufungua fursa mbalimbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi
ikiwa ni pamoja na kuzitilia mkazo ushirikishaji wa wanawake katika uchimbaji
wa madini wenye tija.
Dkt. Biteko amesema hayo Februari 28, 2025 jijini Dar es
salaam wakati aliposhiriki kongamano
maalum kuelekea Maadhimisho Siku ya Kimataifa ya Wanawake (Pre IWD) ambapo
amesema kwa sasa kuna ongezeko kubwa la
wanawake wanaoshiriki katika Sekta ya madini ambayo kwa muda mrefu imekuwa
ikitawaliwa na wanaume na kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,
watu 6,030,575 wanajihusisha na shughuli mbalimbali katika mnyororo wa thamani
katika sekta ya madini.
Kufuatia takwimu hizo, wanawake ni 3,094,647 sawa na
asilimia 51.3 ya watu wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali katika
uchimbaji mdogo wa madini hususan katika sekta ndogo ya u ziduaji. Aidha, kati
ya wachimbaji wadogo milioni moja na nusu, asilimia 27 kati yao ni wachimbaji ni wanawake.
Ametaja jitihada za Rais Samia katika kukuza ushiriki wa
wanawake katika sekta hiyo kuwa ni kutoa kipaumbele wanawake kushiriki katika
shughuli zote za Kiuchumi kwa kuwapa
fursa za elimu pamoja na kumiliki rasilimali zilizopo kama vile kupata
elimu, fursa za kupata mikopo yenye masharti nafuu pamoja na kupata vifaa na
vitendea kazi na kushiriki katika vikao mbalimbali vya maamuzi.
Amefafanua kuwa ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini
ni nyenzo muhimu katika kukuza mnyororo
wa thamani katika jamii na hivyo ni muhimu kutambua na kuthamini mchango wao
katika shughuli hizo na jamii kwa
ujumla.
Aidha, taarifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Sekta
ya Madini ikijumuisha na masuala ya gesi, kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021
imechangia kwa kiasi kikubwa katika ajira. Ambapo ajira za moja kwa moja
218,353. Kati ya ajira hizo, 176,815 ni wanaume na 41,538 ni wanawake ambayo ni
sawa na asilimia 20.
Amesema Serikali imetekeleza na kuweka mazingira wezeshi kwa
wanawake kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo kupitia utekelezaji wa Sera
wezeshi, Sheria na taratibu mbalimbali ambapo kupita Sera ya Taifa ya Jinsia na
Maendeleo ya Wanawake ya mwaka (2023) na Sheria ya Madini ya mwaka (2017)
pamoja na kanuni za ‘Local Content’, Serikali inasisitiza ushirikishaji wa
wanawake na kuhakikisha wanapata uwezo rasilimali katika sekta ya madini.
Vilevile, uwezeshaji wa kifedha na kitaaluma, ambapo
Serikali kupitia Taasisi zake na wadau mbalimbali ikiwemo Kamisheni ya Madini Tanzania na Umoja wa
Wachimba Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA), imesadia kutoa mafunzo ya kitaalam
kwa wanawake mbalimbali ndani na nje ya
nchiambapo mwaka 2023, Serikali iliwapeleka wanawake watano nchini China kwa ajili ya kujifunza na
kutafuta masoko.
“Jumla ya kiasi kisichopungua shilingi bilioni 10
kimeelekezwa katika kuwezesha miradi na shughuli mbalimbali za wanawake wachimba
madini kwa ngazi ya chini. Aidha, katika mitambo ya uchorongaji 10 iliyonunulwa
na Serikali kupitia STAMICO mitambo miwili itakabidhiwa kwa wachimbaji wanawake
kupitia TAWOMA,”amesisitiza Dkt. Biteko.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema ushirikiano wa
sekta ya umma, Sekta binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kuinua ushiriki
wa wanawake katika sekta hiyo muhimu ya uziduaji.
Naye Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amewapongeza
waandaaji wa kutaniko hilo chini ya Christer Mhingo kuendeleza ushiriki wa
wanawake katika sekta hiyo ya uziduaji.
“Bi. Christer amekuwa balozi mzuri wa sekta ya uziduaji
ndani na nje ya nchi, amekuwa
akizitangaza fursa za utalii
zilizopo nchini. Wizara tutaendelea
kumuunga mkono ili atimize malengo yake,” amesema Waziri Mavunde.
Halikadhalika, amemshukuru
Rais Samia kwa kuweka jitihada mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya Sheria
ya mwaka 2017 ambayo yamesaidia kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini kuanzia uchimbaji hadi kuongeza thamani.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema maono ya Rais
Samia ys kuunda inayoshughulikia masuala ya wanawake moja kwa moja ni moja ya
chachu katika ukombozi wa wanawake wakiwemo wale wanaofanya kazi katika sekta
ya madini.
“Mheshimiwa Rais alivyoona kuna umuhimu wa kuwawezesha
wanawake kwa karibu zaidi ndipo akaunda upya Wizara ambayo ndani yake kuna
kipengele kinachoshughulikia masuala ya wanawake. Ndiyo maana tunasema Samia…”
amesema Naibu Waziri Mwanaidi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Azurite Management and Consultancy na waandaji wa tukio la awali kuelekea Maadhimisho ya Siuku ya Wananwake (Pre International Women’s Day), Bi. Christer Mhingo amesema kuwa Taasisi yake iliandaa programu mbalimbali katika maeneo tofauti tofauti na wamekutana na wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari kwa ajili ya kusaidia wanawake waliopo kwenye sekta ya uchimbaji madini.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni