Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake,
wahifadhi wanawake wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapaori Tanzania (TAWA)
wametembelea Pori la Akiba Wamimbiki lililopo katika Mikoa ya Morogoro na Pwani
kwa lengo la kuhamamisha utalii wa ndani.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, iliyofanyika Machi 1,
2025, Afisa Mhifadhi Mkuu, Zuwena Kikoti alisema wahifadhi wanawake wa TAWA
wanaungana na wanawake wote nchini katika kuunga mkono jitihada za Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza
utalii duniani.
"Tumeungana na jitihada hizo kama wanawake kwa
kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Mkoani Morogoro kwa lengo la
kuvitangaza na kuwahamisha wanawake wa Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya jirani
kutembelea hifadhi ya Wamimbiki katika kusheherekea siku ya wanawake
duniani" aliongeza Afisa Mhifadhi Kikoti.
Kwa upande wake, akimwakilisha Kamanda wa Pori la Akiba
Wamimbiki Afisa Utalii, Gregory Kalokole alisema hifadhi ya Wamimbiki ni mpya
na ya kimkakati yenye vivutio vingi vya utalii ikiwemo vivutio vya asili na
vivutio vya utamaduni.
"Pori la Akiba Wamimbiki lina mandhari nzuri
iliyozungukwa na miti ya miombo, wanyamapori kama vile Tembo, Simba, Viboko,
Chui, Fisi, Tandala, Swala pala na Kulo na asilimia takribani 20 ya Mto Wami
umepita ndani ya hifadhi," aliongeza Afisa Utalii Kalokole.
Sambamba na hilo, Kalokole alitoa shukrani zake kwa
wahifadhi wanawake kutembelea hifadhi hiyo na alitoa rai kwa makundi mbalimbali
ya wanawake na watanzania wote kwa ujumla kuja kutembela hifadhi hii.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yamepangwa kufanyika Kitaifa Jijini Arusha Machi 8, 2025 na kauli mbiu ya mwaka huu ni Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.
Na. Joyce Ndunguru - Morogoro
0 Maoni