Wizara ya Maliasili na Utalii na moja ya makampuni makubwa ya utalii duniani ya Abercrombie and Kent Travel Group (AKTG) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kuongeza watalii wa kimataifa nchini Tanzania.
Hayo yamefikiwa jana huko Monaco wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi na ujumbe wake walipokutana na Bi. Christina Levis, Mtendaji Mkuu AKTG.
Abercrombie & Kent Group yenye zaidi ya wafanyakazi 2,500 na ofisi 60 kwenye mabara 7 zaidi ya nchi 36 ina makampuni kadhaa ndani yake yanayotoa huduma mbalimbali za kiutalii duniani.
Baadhi ya makampuni chini ya Mwenyekiti na mmiliki wa AKTG, Manfredi Lefebvre, ni Abercrombie & Kent miongoni mwa kampuni zinazoongoza kusafirisha watalii duniani ikimiliki pia ndege na mahoteli; kampuni ya Crystal Cruises inayomiliki na kusimamia usafiri wa meli za kifahari za watalii na kampuni ya Cox and Kings inayojulikana sana kwa kusafirisha watalii katika makundi kwenda sehemu mbalimbali duniani.
“Tanzania ni moja ya nchi ambako tayari tuna ofisi jijini Arusha na tuna magari kadhaa na kambi ya kulaza wageni Ngorongoro hivyo ni soko letu muhimu ambalo tutafurahi kuendeleza nanyi mikakati ya pamoja kuongeza watalii zaidi,” alisema Bi. Christina.
“Tanzania kwa sasa iko katika hatua kubwa za kuboresha huduma na kutangaza utalii wake. Tunafurahi na tunawakaribisha kuwekeza zaidi Tanzania hasa pia kwa kuwa Mwenyekiti wenu Bw. Manfredi alikutana na Rais wetu wakati wa maandalizi na uzinduzi wa filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour.’
“ Tunajua kwa ukubwa wenu mkiwa mnamiliki na kuratibu safari za ndege, meli za kifahari, maeneo ya malazi na zaidi kusikilizwa kwenu kwenye soko la utalii kwenye mabara yote, mkiungana nasi kimkakati tutafanikiwa kuleta watalii zaidi nchini Tanzania,” alisema Dkt. Abbasi.
Ametumia muda huo pia kuwakaribisha watendaji wa kampuni hiyo kushirikiana na Tanzania katika matukio mawili makubwa mwaka huu ambayo ni Mkutano wa Utalii wa Vyakula Kanda ya Afrika unaoandaliwa kwa kushirikiana na UN Tourism Aprili, 2025 jijini Arusha na Tuzo za Dunia za Utalii, kwa ukanda wa Afrika na Bahari ya Hindi ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji Juni 2025.
0 Maoni