Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kupitia
Mradi wa RISE - Uondoaji wa vikwazo vya barabara umekamilisha Mradi wa
matengenezo ya Barabara ya Songambele - Banyibanyi yenye urefu wa Km 10.
Barabara hiyo inayounganisha Kata za Songambele na Hogoro
inatajwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Kata hizo wanaojishughulisha na
kilimo cha mazao mchanganyiko na ufugaji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Songambele Bw. Said Matonya amesema
kuwa moja ya manufaa ya kukamilika kwa barabara hiyo ni kurahisisha usafiri na
usafirishaji kwa wananchi wa Kata za Songambele na Hogoro.
"Barabara hii imesaidia maeneo yetu mengi ya huduma za
jamii, kwa mfano kilimo ambacho hufanyika maeneo ya magharibi kule kwa hiyo
mazao yanasafirishwa kwa urahisi na kufika masokoni kwa wakati,” amebainisha.
Kwa upande wake Bibi Dora Christopher Samira Mkazi wa Kijiji
cha Songambele amesema hapo awali walipata changamoto hasa kipindi cha mvua
ambapo watoto walikuwa wanashindwa kwenda shule, watu wa maeneo ya Masena
walikuwa wanashindwa kuzifikia huduma za kijamii lakini baada ya mradi huo
huduma nyingi sasa zinafikiwa kwa urahisi ikiwemo huduma ya afya, amefafanua
Bibi Dora.
Mzee Ivan Maswaga Wenga mkazi wa Kijiji cha Songambele kwa
upande wake anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea barabara kwani
barabara hiyo ilikuwa inawazuia wanafunzi kwenda shule ya Msingi Ndachi na
shule ya sekondari Mnywange hivyo ni matumaini yake Sasa kuwa barabara hiyo
itawarahishia vijana wao kupata elimu kwa urahisi.
Naye, Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Kongwa Mhandisi Boniface Mandi amesema kuwa Mradi huo umehusisha matengenezo ya barabara Km 10 na ukarabati wa makavati matano na unapita katika vijiji vitatu Songambele, Masena na Banyibanyi na umekamilika kwa 100%.



0 Maoni