Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga katika
kuendelea kuimarisha na kuboresha uwezo wa Mawakili wa Serikali nchini, hayo
yamesemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari wakati
akizungumza na kwenye Mkutano maalaumu na vyombo vya habari uliofanyika jana katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kivukoni Jijini,
Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali
amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeandaa mafunzo maalumu kwa Mawakili
wa Serikali nchini yatakayofanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 24 hadi 28
Machi, 2025 yakiwa na lengo la kuongeza umahiri na utendaji kazi wa Mawakili
hao.
Mafunzo hayo kwa Mawakili wa Serikali ni sehemu ya
kuimarisha utaratibu wa Mafunzo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa
Mawakili hao, pamoja na utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa Maadhimisho ya
Wiki ya Sheria yaliyofanyika mapema mwezi Febuari, 2025 ambapo aliiagiza Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuboresha na kuimarisha utendaji kazi wa
Mawakili wa Serikali.
“Mhe. Rais amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha inaboresha na kuimarisha uwezo wa Mawakili
wa Serikali ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha," amesema
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mhe. Johari ameeleza kuwa Mafunzo hayo kwa Mawakili
wa Serikali yataendeshwa na wakufunzi wabobezi wa ndani na nje ya nchi, ambao
watatoa mada mbalimbali zitakazo waimarisha mawakili hao katika Uandishi,
Uingiwaji na Majadiliano ya Mikataba ya Kimataifa, Usuluhishi wa Migogoro ya
Kibiashara, na Uandishi wa Sheria.
“Kama mnavvofahamu Mhe. Rais anazidi kuifungua nchi, wigo wa
uwekezaji unaizidi kupanuka hivyo sisi kama Wanasheria ni lazima tuhakikishe
kwamba tunanyumbulika ili kuendana na kasi hiyo.” Ameeleza Mhe. Johari .
Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema
Mafunzo hayo yatatoa fursa kwa Mawakili wa Serikali kujifunza zaidi majukumu
yao katika kuuvaa uzalendo na kulinda maslahi na usalama wa Taifa, ili waweze
kufanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya Taifa na kuzingatia Usalama wa nchi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa, Mafunzo hayo
yatawasaidia Mawakili wa Serikali kuweza kujikumbusha Sheria zinazohusu foreign
exchange, hati fungani na dhamana.
“Tunataka kuwa na Wanasheria na Mawakili ambao watakuwa na
uelewa mzuri katika masoko ya fedha, masoko ya mitaji,” amesema Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Vilevile Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa
Mawakili wa Serikali nchi nzima kuhudhuria bila kukosa mafunzo hayo, huku
akiziomba Wizara, Taasisi na Halmashauri kuwaruhusu na kuwawezesha Mawakili wa
Serikali kushiriki katika mafunzo hayo kwani yatasaidia kuboresha utendaji kazi
wao.
“Nitoe wito kwa Mawakili wa Serikali ambao hawajajisajili
wafanye hivyo haraka sana ili waweze kuhudhuria mafunzo haya ambayo yatawasaida
kuimarisha utendaji kazi wao.” amesema Mhe. Johari.
Sambamba na hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitumia Mkutano huo na Vyombo vya Habari kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne ya Uongozi wake pamoja na mafanikio makubwa ambayo Taifa imeweza kuyapata.
0 Maoni