WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema jamii inahitaji
kufundishwa, kutambua na kuenzi mila za Kitanzania, pamoja na kujiepusha na
vishawishi vya kuiga tabia za kigeni ambazo hazina manufaa kwa ustawi wa Taifa.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Machi
19, 2025) katika Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Msaidizi Mstaafu wa
Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Bukoba Askofu Method Kilaini.
“Sote tumekua tukishuhudia ongezeko la vitendo vya ukosefu
wa maadili katika jamii. Vitendo hivi vinatokana na malezi hafifu lakini pia
watu kuiga mila na desturi kutoka mataifa mengine ambazo haziendani na tamaduni
na maadili yetu ya Kitanzania.”
Waziri Mkuu amesema hali hiyo imeathiri mwenendo wa jamii,
hususan kwa vijana ambapo wanashuhudia mabadiliko katika misingi ya familia,
jamii, na Taifa kwa ujumla. “Nitumie fursa hii kuliomba Kanisa kuendelea kuwa
nguzo ya maadili bora, kwa kutoa mwongozo wa kiroho na kijamii.”
Amesema Kanisa lina nafasi ya pekee katika kuhakikisha Taifa
linarudisha maadili ya kweli ya Kitanzania yanayofundisha kuheshimu utu, haki,
na amani. “Serikali, tunatambua mchango mkubwa wa Kanisa katika hili na
tutashirikiana nalo ili kuleta mabadiliko chanya kwa kizazi cha sasa na
kijacho.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inatambua na
kuthamini mchango wa madhebu ya dini ikiwemo Kanisa Katoliki katika kuboresha
ustawi wa jamii.amii yetu., hivyo amewaomba viongozi wa dini nchini waendelee
kuwa nguzo ya maadili bora, kwa kutoa mwongozo wa kiroho na kijamii.
Akizungumza kuhusu Askofu Kilaini, Mheshimiwa Majaliwa
amesema ni kielelezo cha ujasiri, imani thabiti, na huduma ya kujitolea kwa
Kanisa na jamii ya Watanzania, ameonesha nguvu ya uvumilivu, akiwa na michango
mikubwa katika maisha ya kanisa.
Amesema pamoja na changamoto nyingi alizokutana nazo,
hakukata tamaa, bali aliendelea kuwa mwanga kwa wengi. “Ninatambua kuwa katika
kipindi cha uongozi wake, alifanya kazi muhimu katika Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania, akiwa Katibu Mkuu kwa miaka tisa na nusu, akisaidia
kuimarisha huduma za jamii na kuendeleza taasisi mbalimbali za Kanisa, ikiwemo
hospitali ya Bugando na Chuo Kikuu cha Nyegezi.”
“Kama Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
alijizatiti katika kuimarisha utawala wa fedha za Kanisa na kusaidia kuanzisha
Radio Tumaini, hatua muhimu katika mawasiliano ya kiroho. Kwa ushirikiano wake
na viongozi wa Kanisa, alisaidia pia kuanzisha Television ya Tumaini, akionesha
uongozi wa kimapokeo na kisasa.”
Akimzungumzia Askofu Msaidizi Mstaafu. Method Kilaini Mkuu
wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwasa amesema Askofu huyo ni hazina kubwa ya mkoa wa
Kagera kwani licha ya kutoa huduma za kiroho mara nyingi amekuwa akishiriki
katika matukio mabalimbali yanayofanywa na Serikali. "Amekuwa mshauri
mzuri katika masula mbalimbali hasa yanayohusu amani na maendeleo ya Taifa
letu.”
Naye, Balozi wa Baba Mtakatifu nchini, Askofu Mkuu Angelo
Accaltino amesema anafurahishwa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya kanisa
Katoliki na Serikali ya Tanzania na uwepo wa Mheshimiwa Waziri Mkuu katika
Jubilei hiyo ni ushahidi. “Natamani kuona ushirikiano huu unadumu na kuendelea
kukua.”
Kwa upande wake,
Askofu Msaidizi Method Kilaini amesema anamshukuru Mungu kati ya mambo
mengi aliyoyafanya aliguswa sana na ushirikiano alioupata kutoka kwa Sheikh wa
Mkoa wa Kagera Haruna Kichwabute katika kutafuta amani na maridhiano kati ya
Wakristo na Waislamu mkoani Kagera.
“Tumefanikiwa sana kuwaunganisha Wakristo na Waislamu mkoani kwetu, sisi ni ndugu sisi ni wamoja na ndio maana leo hii namuona Sheikh wetu wa Mkoa yupo hapa kanisani akishirikiana nasi katika Jubilei hii.”
0 Maoni