MGODI wa Dhahabu
wa Manda, unaomilikiwa na Wakinamama chini ya uenyekiti wa Asha Msangi
umechangia Shilingi Milioni 800 katika maduhuli ya Serikali kwa mwaka huu wa
fedha 2024/2025.
Mgodi huo
ambao kwa kiasi kikubwa unaendeshwa na wakinamama upo Kahama Kijiji cha Mwime
Kata ya Zongamela ambao una leseni ya uchimbaji mdogo wa madini na umeajiri
zaidi ya vijana 200.
Akizungumza
katika mahojiano mmiliki wa mgodi huo ambae pia ni Mwenyekiti wa wanawake
wachimbaji mgodini hapo, Asha Msangi anasema “Kabla ya kuanza kwa shughuli za
uchimbaji wa madini nilikuwa nafanya biashara ndogo ndogo, nilikuwa na kiduka
kidogo tu, badae nikahamia kwenye mazao nikawa napeleka mchele Arusha hata
hivyo biashara ilikuwa ngumu, nikahamia kwenye uchimbaji.”
“Nilikuwa
nachimba kwenye migodi ya watu, nikapata uzoefu nikaomba leseni nikapewa moja
kama majaribio lakini nashukuru nilifanya vizuri na nikaaminika sasa hivi
namiliki leseni 12, nimeunda na vikundi vya kinamama ambao nashirikiana nao
kuchimba,” amesema Asha.
Kwa
upande wa Afisa Madini Mkazi wa Kahama,
Leons Welengeile amesema mgodi huo wa
Manda ni wadau muhimu na unatoa ajira
kwa vijana na kinamama wengi kupitia shughuli zinazoendelea katika mgodi huo.
“Kwa mwaka
huu wa fedha 2024/2025 kuanzia mwezi Julai 2024 hadi Februari 2025 mgodi huu wa
Manda umechangia Shilingi Milioni 810 katika maduhuli ya Serikali na hiyo ni
kupitia mrabaha na tozo ya ukaguzi ambazo zinakusanywa na Tume ya Madini
Kahama, achilia mbali makusanyo mengine yaliyokusanywa na halmashauri na
TRA,”amesema Leons na kuongeza,
“Kwa hiyo
tuwaamini wakina mama, hivyo tunaendelea kufungua fursa kwao,”amesisitiza.
Aidha, Leons
amesema maduhuli ya Serikali katika Mkoa wa Kimadini Kahama yameendelea kupanda
mwaka hadi mwaka kutoka ukusanyaji wa Shilingi
Bilioni 97 mwaka 2022/2023, Shilingi Bilioni 101 mwaka 2023/2024 na kwa
mwaka 2024/2025 hadi mwezi Machi 2025 kiasi cha Shilingi Bilioni 88.08
kimekusanywa ikiwa ni sawa na asilimia 85 ya makusanyo ya Miezi 9,”amesema.
Amesema
anaamini kwa mwelekeo unavyokwenda mpaka
kufikia mwishoni mwa mwaka wataweza kutimiza
lengo la makusanyo kama ilivyokusudiwa.



0 Maoni