Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amemtaka Meneja wa
Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold
Runji, kuhakikisha wakandarasi wanakamilisha ujenzi wa barabara za lami
Ikwiriri ndani ya miezi miwili ili wananchi wanufaike na maboresho ya
miundombinu hiyo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Mhe.
Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua
maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo wilayani Rufiji.
"Natoa miezi miwili tu, barabara ziwe
zimekamilika ifikapo Mei 30, 2025, ikiwa ni pamoja na mitaro na taa za
barabarani. Hakutakuwa na nyongeza ya muda," amesisitiza Waziri
Mchengerwa.
Ameagiza
Meneja wa TARURA kuwasimamia wakandarasi wafanye kazi usiku na mchana,
akibainisha kuwa barabara hizo zilipaswa kukamilika Desemba 2024 na iwapo
hazitakamilika kwa muda uliopangwa, atamuwajibisha meneja huyo.
Nao, Baadhi
ya wananchi, akiwamo Dereva wa bodaboda Ramadhan Mwipi na Mama Lishe Mariam
Hamza, wamemshukuru Waziri Mchengerwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuboresha barabara hiyo, wakieleza kuwa imeleta ahueni kubwa kwa usafiri
na biashara zao.



0 Maoni