WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa
uzalishaji mazao ya misitu kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao hayo hapa nchini
badala ya kusafirisha malighafi hizo nje ya nchi.
Amesema kuwa Tanzania kwa sasa inayo teknolojia kubwa ya
uchakataji wa mazao ya misitu na utengenezaji wa Samani zake hivyo hakuna haja
ya wadau wa misitu kusafirisha mazao hayo kwenda nje kwa ajili ya uchakataji.
"Lazima tuweke ukomo wa uvunaji na uchakataji tunataka
kila kitu wamalize hapa hapa kama wanavyofanya TANWAT, wanaanza mwanzo mpaka
mwisho wakiwa hapa hapa Tanzania, hapa hapa njombe kwa hivyo na viwanda vingine
vibainishwe ambavyo havijakamirisha, tulishawapa muda inatosha".
Ameyasema hayo leo, (Ijumaa 21, Machi, 2025) katika kilele
cha maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa
yaliyofanyika Mkoani Njombe.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Maliasili na
Utalii, kuendelea kuhamasisha na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika
kuanzisha mashamba ya miti na viwanda vya kuongeza thamani mazao ya
misitu.
Kadhalika ameitaka Wizara hiyo kushirikiana na Mamlaka
nyingine kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu kuhusu uhifadhi na biashara
ya kaboni ili waweze kuanza kunufaika kupitia biashara hiyo.
"Taasisi za misitu ziweke mipango thabiti ya
kukabiliana na uchomaji moto ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia teknolojia
katika kutambua na kupambana na moto."
Pia amezitaka, Wizara na Taasisi hizo kuhakikisha
zinaboresha ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa sekta ya misitu na jamii
inayozunguka maeneo ya misiti ili kuhakikisha mipango na mikakati ya uhifadhi
inatekelezwa kwa ufanisi.
"Wataalamu wa misitu wanapaswa kushirikiana na jamii
katika utekelezaji wa miradi ya uhifadhi, ikiwemo kuanzisha mashamba ya misitu,
na programu za upandaji miti."
Awali, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea kiwanda cha uchakataji mazao ya misitu cha TANWAT (Tanganyika Wattle Company Limited) kilichopo Njombe mjini ambapo alishuhudia shughuli mbalimbali zinazofanywa na kiwanda hicho.
0 Maoni