Kamati ya kudumu ya Bunge ya uwekezaji wa mitaji ya Umma
(PIC) imefanya ziara katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro tarehe 23-24 Machi,
2025 na kuipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa uboreshaji wa miundombinu
ya Utalii na ujenzi wa jengo la Makao makuu ya NCAA nje ya Hifadhi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya uwekezaji wa mitaji ya Umma
Mhe. Augustine Vuma (Mb) amesema kuwa, kamati inaipongeza NCAA kwa ujenzi wa
Jengo la Makao makuu ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha shughuli
za uhifadhi na kupunguza shughuli za kibinadamu katika hifadhi ya Ngorongoro.
“Kamati ya PIC imekagua jengo hili na miundombinu mingine ya
utalii, tunawapongeza kwa ujenzi wa jengo hili lenye kiwango kinachoendana na thamani
ya fedha, hakikisheni mnamsimamia mkandarasi kumaliza ujenzi huu kwa wakati ili
jengo hili lizinduliwe naa kutumika kwa kazi za Mamlaka na kutimiza kusudio la
Serikali la kuboresha uhifadhi na kupunguza shughuli za kibinadamu ndani ya
hifadhi,” alisisitiza Mhe. Vuma.
Wabunge wa Kamati hiyo wameipongeza NCAA kwa uboresjaji wa
miundombinu ya utalii na kutangaza vivutio vya utalii hali iliyopelekea
ongezeko la Mapato ambayo yanapoingia kwenye mfuko mkuu wa Serikali yanasaidia
kuwekeza katika miradi mingine na kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi.
Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi wa NCAA Jenerali Venance Mabeyo (mstaafu) ameielezea kamati hiyo
kuwa Bodi na menejimenti ya NCAA itaendelea kuhakikisha kuwa miundombinu inayojengwa
ikiwemo jengo la Makao makuu na miradi mingine inasimamiwa kikamilifu na
kufanyiwa maboresho ya mara kwa mara ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wageni
wanaotembelea NCAA.
Akitoa taarifa ya Mradi, Meneja wa Mradi huo Mhandisi Humphrey Swai ameeleza kuwa ujenzi wa jengo la Makao makuu ya NCAA unaotekelezwa na kampuni ya China Jiangxi for International Economic and Technical cooperation Co. Ltd umegharimu shilingi Bilioni 10,474,526,694.25 ambapo fedha hiyo imehusiaha ujenzi wa jengo la Makao makuu, Nyumba ya kamaishna wa Uhifadhi na Nyumba mbili za manaibu Kamishna wa Uhifadhi ambapo ujenzi umeshafikia asilimia 85 na ujenzi unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Mei, 2025.
0 Maoni