Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua taarifa ya Utendaji
wa Mamlaka za maji kwa mwaka 2023/24 na kusema upatikanaji wa huduma za maji ni
haki ya msingi hivyo ni muhimu kulinda vyanzo vya maji kuwezesha upatikanaji
wake.
Dkt. Biteko
amesema hayo jijini Dar es Salaam Machi 19, 2025 ambapo amesema pamoja na
jitihada zinazoendelea jamii ina wajibu wa kuhakikisha usafi wa mazingira,
kupanda miti na kuhifadi misitu ili kuendelea kupata na kutumia rasilimali
maji.
“Tusipotunza
vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira tutajikuta katika mtanziko mkubwa (water
Stress),” amesema na kuongeza kukosekana kwa rasilimali maji kwa baadhi ya watu
kinaweza kuwa chanzo cha migogoro na machafuko katika jamii husika.
Ili
kukabilikana na hali hiyo na kumwezesha kila Mtanzania kupata huduma za maji na
usafi wa mazingira, Dkt. Biteko amezielekeza mamlaka za maji kupunguza kiwango
cha upotevu maji ili kuepusha hasara ya shilingi bilioni 114.12 iliyotokana na
upotevu huo kwa mwaka huu.
Hadi sasa
asilimia 84 kwa mijini na asilimia 79.6 kwa maeneo ya vijijini zimeunganishwa
na huduma ya maji ambapo kuna ongezeko la asilimia 7 kutoka kipindi cha mwaka
uliotangulia.
Awali, Waziri
wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema kumekuwa na ongezeko la ubora wa viwango vya
maji na udhibiti wa upotevu wa maji ambao unasababisha hasara kubwa hasa
unapothamanishwa kifedha.
Hata hivyo
ameipongeza EWURA kwa kazi nzuri na kutoa taarifa inayoonesha uhalisia wa mambo
huku akisema mamlaka zinazofanya vizuri zinapata tuzo ikiwa ni motisha ya
ushindani wa kimaendeleo.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Profesa Mark Mwandosya ameipongeza Serikali
kwa kuendelea kutoa kipaumbele na kuongeza bajeti ambayo imeongezeka kutoka
shilingi bilioni 206 mwaka 2010/11 hadi shilingi bilioni 558 mwaka 2024/25.
Amesema
uwekezaji wa katika sekta ya maji unaleta faida zaidi ya mara saba ya mtaji
ambapo uwekezaji wa dola 1 unaweza kuleta faida ya dola 7 katika Uchumi wa
taifa.
Mkurugenzi
Mkuu wa EWURA Dkt. James Andelile amesema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa bado
kuna changamoto kadhaa zinazotokana na utegemezi wa Mamlaka za maji kwa
Serikali.
Pia amesema
changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu ya maji inayosababisha upotevu
wa maji na hasara kwa serikali.
Mamlaka za
maji zilizofanya vizuri katika udhibiti wa upotevu wa maji na asilimia ya maji
yanayopotea ni Maganzo 4%, Nzega 6%, Kashuwasa 11%, Biharamulo 12% na Mwanuzi
13%.
Mamlaka
zilizoshindwa kudhibiti upotevu huo kwa kiwango kikubwa ni Rombo 70%, Handeni
69%, Mugango/kyabakari 68%, Ifakara 56% na Kilindoni 55%.
Dkt. Biteko
akiwa Mgeni rasmi ametoa tuzo na vyeti kwa mamlaka za maji zilizofanya vizuri
katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni