Balile achukua fomu kuwania tena Uenyekiti TEF

 

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile amechukua fomu ya kuwania tena nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka minne, ikiwa zimebaki siku 15 kabla ya kufanyika uchaguzi wa viongozi wa TEF.

Balile amechukua fomu leo tarehe 21 Machi 2025 katika ofisi za TEF zilizopo Kisutu Jijini Dar es Salaam kutetea nafasi hiyo, huku akisindikizwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho.

Uchaguzi wa TEF utafanyika tarehe 5 Aprili 2025 Songea mkoani Ruvuma ambapo utatanguliwa na Mkutano Maalum utakaoanza tarehe 3 Aprili 2025.

Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi.

Balile amekuwa Mwenyekiti wa jukwaa hilo baada ya kushinda kwenye uchaguzi uliofanyika mwaka 2021.

Jumla ya wagombea 14 tayari wamechukua fomu za kugombea ambapo katika nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF wamechukua wagombea 12, nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti zina mgombea mmoja mmoja.

Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Jumatatu tarehe 24 Machi 2025.



Chapisha Maoni

0 Maoni