Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua
kuwekeza kwenye ufundi ili Watanzania waweze kujikomboa katika uchumi.
Hayo
yamebainishwa leo Machi 21, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,
Mhe. Dkt. Doto Biteko akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya miaka 50
ya utoaji Elimu na Mafunzo ya ufundi Stadi nchini (VETA) iliyofanyika jijini
Dar es Salaam.
Dkt. Biteko
amesema kuwa, Serikali imeweka msukumo mkubwa katika ufundi stadi ili
Watanzania wapate elimu yenye viwango vikubwa na ujuzi wa kuweza kujikomboa
katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
"Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anajenga VETA
kila wilaya ili kuwapa ujuzi watanzania waweze kuajirika katika sekta
zote," amesisitiza Dkt. Biteko.
Aidha,
ameipongeza Mamlaka ya elimu na mafunzo
ya ufundi stadi (VETA) kwa kuwa na
maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa
hatua hiyo kubwa na kuwataka kuendelea kufanya kazi ili kuwajengea uwezo
watanzania katika ujuzi mbalimbali.
"Kwa
mara myingine nawapongeza VETA kwa kuendelea kutoa mafunzo na ujuzi kuendana na
mabadiliko ya teknolojia ili kuhakikisha kuwa ujuzi unatolewa kwa kuzingatia
ubora na viwango vya kimataifa, " amesema Dkt. Biteko.
Vile vile,
amesisitiza elimu kutolewa kwa watu wenye mahitaji maalumu na wanaotoka kwenye
mazingira magumu nchini yaweze kuongeza fursa kwa kila mtanzania kupata elimu
ya ujuzi.
Naye, Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kwamba, Maadhimisho
ya Miaka 30 ya VETA ni uhalisia kuwa Serikali imeipa kipaumbele VETA ili vijana
wapate elimu ikiwemo kujenga vyuo vya ufundi katika maeneno mengi nchini.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA, Anthony Kasore amesema kuwa, VETA imezingatia
viwango na ubora wa mafunzo unazingatiwa ili vijana wanaohitimu waweze kumudu
soko la ajira. Aidha amemshukuru Rais Samia kwa usimamizi na uwezeshaji wake
mkubwa katika mafunzo ya ufundi stadi nchini ili vijana waweze kupata maarifa
na ujuzi ya kufanya shughuli za kiuchumi kwa tija.




0 Maoni