Mahakama ya Wilaya Bariadi mkoani Simiyu imemhukumu kifungo
cha miaka 20 jela pamoja na kuchapwa viboko 12 Emmanuel John (31), maarufu kama
Chief wa Kilulu, kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali aina ya fisi akiwa
hai na akiishi naye nyumbani kwake.
Mshtakiwa huyo, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kilulu
kilichopo kata ya Bunhamala, wilayani Bariadi, na mganga wa kienyeji, alipewa
adhabu hiyo katika kesi namba 2458/2025 iliyokuwa ikimkabili kwenye mahakama
hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
hiyo, Caroline Kiliwa, mara baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na
upande wa mashtaka.
Awali, akisoma kosa la mshtakiwa, Mwendesha Mashtaka kutoka
Ofisi ya Mashtaka Mkoa, Lupiana Mahenge, alieleza Mahakama kuwa mtuhumiwa huyo
alikutwa na nyara ya serikali, fisi akiwa hai, akimfuga nyumbani kwake kinyume
cha sheria.
Alisema kuwa mnamo Januari 1, 2025, katika eneo la kijiji
cha Kilulu, mtuhumiwa alikamatwa kufuatia Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka
kwa raia wema, ambao waliripoti kuhusu mtuhumiwa kuishi na fisi hai ndani ya
nyumba yake.
Alieleza kuwa mtuhumiwa aliishi na fisi huyo kama mnyama wa
kufuga kinyume na kifungu cha 86 (1) na kifungu kidogo cha (2)(C)(III) cha
Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori sura ya 283, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka
2022.
Alisema kuwa kifungu hicho kinasomeka pamoja na kifungu cha
14, jedwali la kwanza na kifungu cha 57 (1), na kifungu cha 60 (2) cha Sheria
ya Kupambana na Uhujumu Uchumi sura ya 200, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka
2022.
Upande wa mashtaka, katika kuthibitisha kosa hilo, ulipeleka
mashahidi sita ambao waliithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka.
Mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliomba Mahakama imsamehe kwa kuwa anategemewa na familia ya watoto wanne, wakiwemo mapacha, ndipo hakimu akatoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela na viboko 12 ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine.
Chanzo: Global TV
0 Maoni