Watalii kutoka nchi ya Ubelgiji waongezeka kutoka 5,374 hadi 17,825

  

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Jestas Nyamanga ameeleza kuwa watalii 17,825 kutoka Nchi ya Ubelgiji wametembelea vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania mwaka 2023.

Mhe. Balozi Nyamanga ameeleza hayo wakati akizungumza na Wakala wa Utalii kutoka nchi ya Ubelgiji ambao wamekutana na Wakala wa Utalii kutoka Tanzania wakati wa msafara wa utangazaji Utalii ujulikanao kama "My Tanzania Roadshow, Europe 2025."

Balozi ameeleza kuwa idadi ya Watalii kutoka Ubelgiji imeendelea kuongezeka hasa baada ya janga la Covid-19 ambapo mwaka 2020 watalii kutoka nchi hiyo walikuwa 5,364 pekee. Ni kutokana na mikakati thabiti ya utangazaji inayoendeshwa na taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, na ushirikiano baina yao na ofisi yake idadi ya  watalii imeongezeka kwa kasi na kufikia 17,825 mwaka 2023.

Mhe. Balozi ameongeza kuwa Nchi ya Ubelgiji ni miongoni mwa nchi 15 zinazoleta wageni wengi zaidi Tanzania na kuongeza kuwa "Ubalozi wa Tanzania nchini Ubelgiji utaendelea  kutanganza vivutio  vilivyopo Tanzania kwa kufanya kazi kwa karibu na Wakala wa Utalii waliopo nchi za Ulaya."

Katika hotuba yake Mhe. Balozi aliwataka Wakala hao, mbali ya kushawishi watalii kutembelea Tanzania, wachangamkie fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii, na sekta nyingine za kiuchumi nchini.

Amebainisha kuwa Serikali chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara.

Akihitimisha hotuba yake Mhe. Balozi aliipongeza Kampuni ya Kili Fair iliyoandaa Msafara huu, kwa kushirikiana na Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii za TTB, TANAPA, na NCAA.

 
  

Na. Mwandishi Maalum- Antwerp Ubelgiji

Chapisha Maoni

0 Maoni