Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Machi 12, 2025 ameweka jiwe la msingi la Mradi wa Upanuzi wa Mtandao wa Majisafi ya Ziwa Victoria kutoka Makomero - Mgongoro, uliopo kijiji cha Mwamayoka, Igunga mkoani Tabora ambao umegharimu shilingi milioni 840.8.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, ambao unatarajia
kuhudumia wananchi 5,402, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea
kusimamia utoaji wa huduma za maji safi na salama nchini ili kuhakikisha hali
ya upatikanaji wa maji inawafikia wananchi kwa asilimia 100.
“Ndugu zangu wananchi, mradi huu ni matokeo ya utekelezaji
wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, kuweni na uhakika kwamba Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan ni kiongozi
anayewajali, anawapenda na anasikiliza changamoto zenu, endeleeni kutekeleza
majukumu yenu ipasavyo kwasababu tunaye kiongozi madhubiti.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza RUWASA kuongeza na
kusogeza vituo vya kuchotea maji karibu na wananchi “RUWASA hakikisheni miradi
hii inatoa maji wakati wote.”
Mradi huo ambao umefikia asilimia 80 ya ujenzi unahusisha
ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji, Ukarabati wa vituo sita vya kuchotea
Maji, Ukarabati wa Manywesheo mawili ya Mifugo, kuchimba mitaro ya kulaza bomba
na kufukia mitaro mita 25,000.
Mheshimiwa Majaliwa yupo mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
0 Maoni