Naibu Waziri
wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amevitaka
vyombo vya habari nchini kuwa mstari wa mbele katika kutumia Kiswahili sahihi,
ili kujenga jamii inayozungumza lugha fasaha ya Kiswahili.
Mhe. Mwinjuma
ametoa kauli hiyo jana Februari 14, 2025 Jijini Dodoma wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa Vyombo
vya Utangazaji 2025 uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Februari 13-14, 2025.
“Ni rai yangu
kwenu kwa kuwa nyinyi ndio wenye jukumu la kwanza kabisa la kuhakikisha matumizi
sahihi ya Kiswahili ndio yanayoshika hatamu.. Kiswahili sahihi kinatumika
katika vyombo vya habari na hivyo kuambukiza jamii yeu,” alisema Mhe. Mwinjuma.
Pamoja na
mambo mengine, Mhe. Mwinjuma alipongeza mkutano huo kuzungumzia mada mbalimbali
muhimu zikiwemo za Sheria na kanuni za uchanguzi mkuu pamoja na matumizi sahihi
ya akili unde na kusema kwamba milango ya wizara ipo wazi wakati wowote kwa
vyombo vya habari.
Amewataka
waandishi wa habari kutumia mafunzo waliyopatiwa katika mkutano huo kuripoti
uchangizi mkuu wa 2025 kwa weledi wa hali ya juu na kutenda haki ili wananchi
wapate taarifa na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi.
Amesema
kupitia vyombo hivyo wananchi wanapata taarifa sahihi za wagombea
zinazowawezesha kufanya maamuzi kwa mustakabali wa nchi hivyo vina umuhimu
katika uchaguzi ujao wa Oktoba mwaka huu.
Kwa upande
wake Meneja wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka
aliwapitisha washirika katika kufahama kanuni za utangaji za uchaguzi, na
kusisitiza vyombo vya habari kutenda haki kwa vyama vyote.
“Vyombo vya
habari vinapaswa kutenda haki kwa kutoa habari kwa usawa kwa wagombea wote wa vyama vyama vya siasa bila upendeleo wowote
wakati wa uchaguzi mkuu,” alisisitiza Mhandisi Kisaka.
Amesema hata
katika taarifa za habari kila chama kinapaswa kuwa na habari ya kwanza na sio
kila siku chama kimoja tu ndio kinakuwa na habari ya kwanza (lead story) na
kuwataka waandishi wa habari wajikite zaidi katika sera za vyama na ahadi za
wagomea.
“Muepuke
kuripoti habari za wagombea za matusi na lugha za uchochezi, bali mjikite
katika kutoa habari za sera na ahadi za wagombea, pia mjiepushe kuongeza maneno
yenu kwenye habari za kampeni wakati wa uchaguzi,” alisema Mhandisi Kisaka.
Ameeleza kwa
vipindi vya mahojiano wagombea wote wa urais wanapaswa kufanyiwa kwa usawa na iwapo
kuna mdahalo wa wagombea urais, wagombea washindane kwa Ilani za vyama vyao, Sera
na ahadi na wala sio malumbano, na muongozaji hapaswi kuongeza neno lolote baada
ya kumalizika mdahalo.
Mkutano huo
ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) unaofanyika Jijini
Dodoma unakauli mbiu isemayo, “Wajibu wa Vyombo vya Utangazaji Kuelekea
Uchaguzi Mkuu”.
0 Maoni