Mganga Mkuu wa Halmashuri ya Mji wa Babati Mkoani Manyara Dkt. Nassib Msuya ametoa wito kwa Watoa Huduma za Afya kuendelea kutumia takwimu kwa usahihi ili kuleta matokeo chanya katika Huduma za Chanjo.
Dkt. Msuya amebainisha hayo katika Halmashauri ya Mjini
Babati wakati akifunga Mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Watoa Huduma
za Afya katika Halmashauri hiyo juu ya uboreshaji wa Mawasiliano kati ya Mtoa
huduma na Mteja (Interpersonal Communication-IPC)
“Suala la Takwimu ni muhimu muhimu sana hivyo,
tunapotekeleza huduma za chanjo kwa jamii zetu lazima tuhakikishe takwimu za
chanjo zinakuwa sahihi ili pawe na matokeo chanya,”amesema.
Aidha, Dkt. Msuya amesema mahusiano mema na jamii yana
umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa Huduma za afya ikiwemo huduma za chanjo.
“Anapokuja mtu kupata huduma ,lazima kuonesha hali ya
kumsaidia au wewe unapopeleka huduma za chanjo kwenye jamii Fulani jambo la
kwanza zingatia mahusiano mazuri ili afurahie hiyo huduma jitahidi kumfafanulia
kwa undani zaidi faida zake,”amesema.
Afisa Programu wa Mafunzo, Uhamasishaji, na Uelimishaji
Jamii kutoka Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Chanjo Lotalis Gadau amesema
kupitia Mafunzo hayo itarahisisha Watoa Huduma za Afya kuongeza ufanisi wa
utendaji kazi katika maeneo yao.
“Kupitia Mafunzo haya itarahisisha Watoa huduma kuona ni
wapi inatakiwa kufanyiwa kazi ili kuongeza wigo wa huduma katika maeneo yenu ya
Kazi,”amesema Gadau.
Mafunzo ya kuwajengea uwezo Watoa Huduma za Afya katika
Halmashauri ya Mji wa Babati juu ya uboreshaji wa Mawasiliano kati ya Mtoa
huduma na Mteja (Interpersonal Communication-IPC) yamechagizwa na mada
mbalimbili zikiwemo, Umuhimu wa Kuhusisha Jamii ikiwemo kutumia mikutano ya
jamii, Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Matumizi Sahihi ya takwimu.
Mada nyingine ni pamoja na hatua za kuchukua unapopata mgonjwa wa ulegevu/Ulemavu wa ghafla na hatua hizo ni pamoja na kuchukua taarifa muhimu zinazohusiana na mtoto ikiwa ni pamoja na umri, jinsia, jina la mzazi au mlezi, mahali anapoishi, namba ya simu.
0 Maoni