SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania - TAWA imekabidhi madawati 295 yenye thamani ya Shillingi Millioni
25.9 Kwa shule za sekondari na msingi Mkoani Simiyu hatua inayolenga kuboresha
mazingira ya elimu kwa shule zinazozunguka Pori la Akiba Maswa kama sehemu ya
ujirani mwema kati ya TAWA na jamii.
Akizungumza na
waandishi wa habari Februari 7, 2025 mkoani humo Afisa Habari wa TAWA Beatus
Maganja amesema TAWA Kwa kushirikiana na Kampuni ya uwindaji wa kitalii BUSHMAN
SAFARI TRACKERS wametoa madawati 295, meza (2) na viti viwili (2) Kwa shule za
msingi na sekondari zilizopo wilaya za Itilima na Bariadi ambapo wilaya ya
Itilima imepata madawati 190, meza 1 na kiti kimoja (1) na wilaya ya Bariadi
imepata madawati 105, meza 1 na Kiti kimoja (1).
Maganja amesema TAWA imekuwa na utaratibu wa kurejesha faida
zinazotokana na shughuli za uhifadhi kwa jamii
zinazozunguka maeneo ya hifadhi
zilizo chini ya usimamizi wa taasisi hiyo, na kwa Mkoa wa simiyu
madawati hayo yametokana na mapato yanayotokana na shughuli za uhifadhi
zinazofanyika katika Pori la Akiba Maswa.
Aidha, amewaomba wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuendelea
kushirikiana na Serikali katika kulinda rasilimali zilizopo mkoani humo ili
kuendelea kufaidi matunda yatokanayo na rasilimali hizo Kwa faida ya kizazi
kilichopo na vizazi vijavyo.
Kwa upande wao Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Lung'wa
Exavery Lusajo Mwasomola na Mwalimu Stephano Palangyo wameshukuru kwa msaada wa
madawati 100 na kukiri kuwa umesaidia kutatua changamoto ya upungufu wa
madawati kwa asilimia 100 na kuzidi kuomba msaada zaidi wa kujengewa
hosteli, maabara na nyumba za walimu.
Nao wanafunzi wa
shule ya Lung'wa iliyopo wilaya ya Itilima wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
madawati hayo ambayo wamesema yatawasaidia kusoma Kwa ufanisi zaidi na kuongeza
ufaulu wao katika mitihani.
"Sisi wanafunzi wa shule ya Lung'wa tumefurahi sana kupata huu msaada wa viti na madawati, kabla hatujapata madawati tulikuwa tunahangaika sana kwa kukaa chini na wakati mwingine unamkuta mwanafunzi amebeba kiti chake anatembea nacho wakati wa mapumziko yote hiyo ni kutokana na uhaba wa madawati," amesema nchama lusalo sipewa mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Lung'wa wilayani Itilima.
0 Maoni