Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema uwekezaji wa Kituo cha Kisasa cha Ukaguzi na Upasishaji wa Vyombo vya Moto ni mapinduzi makubwa katika Sekta ya Usafiri hapa nchini.
Rais Dkt. Mwinyi
ameyasema hayo alipozungumza katika ufunguzi wa kituo hicho Kwasilva kiliopo
Dole Kizimbani Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kituo hicho
ambacho ni ubia baina ya Serikali na Kampuni ya Kizalendo ya Zenj General
Mechandize kina uwezo wa kuhudumia vyombo vya moto takribani 300 kwa siku kwa
kutumia mashine na teknolojia ya ukaguzi yenye viwango vya Kimataifa.
Aidha, Dkt. Mwinyi
ameeleza kuwa kituo hicho ni muhimu kwa Ukuaji na Maendeleo ya Sekta ya Usafiri
na kitafungua Ukurasa Mpya wa Usalama wa Usafiri Barabarani.
Halikadhalika
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuthamini na kushirikiana
na sekta binafsi kufanikisha miradi ya Uwekezaji ya ndani na ile inayotoka nje
ya nchi kwa mafanikio makubwa.
Akizungumzia
usafiri wa umma Dkt. Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kuwa na Usafiri wa mabasi
ya kisasa ya umeme yatakayotoa huduma bora kwa wananchi.
Akiwasilisha taarifa
ya kitaalamu ya mradi huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi, Habiba Hassan amesema mradi huo wa ubia baina ya Kampuni ya Zenj
General Mechandise na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umegharimu kiasi cha Shillingi
Bilioni 2.8 hadi kukamilika kwake na una uwezo wa kukagua vyombo vya moto 300
kwa siku.
0 Maoni